MASOMO YA MISA, JUNI 18, 2026
ALHAMISI, JUMA LA 11 LA MWAKA
SOMO 1
YbS. 48:1 – 14
Ndipo aliposimama Nabii Eliya,
kama moto, hata na neno lake likawaka kama tanuru. Yeye alileta njaa juu yao,
na kwa juhudi yake akawapunguzia hesabu yao; kwa neno la Bwana akazifunga
mbingu, na mara tatu kutoka huko akatelemsha moto.
Jinsi ulivyotisha kwa miujiza
yako! Aliye mfano wako ataona fahari. Aliyekufa ulimfufua katika mauti, Kutoka
kuzimu, kwa neno la Bwana. Ukawashusha wafalme mpaka shimoni, na watu wateule
vitandani mwao. Ukapaka mafuta wafalme kwa kisasi, na nabii ili akufuate nyuma
yako. Ulisikia makaripio huko Sinai, na hukumu za kisasi huko Horebu.
Ukachukuliwa juu katika kisulisuli, katika gari la farasi wa moto. Ukaandikiwa
kuwa utaleta makemeo, ili kutuliza hasira siku ile ya Bwana; kugeuza moyo wa
baba umwelekee mwana na kuhuisha kabila za Israeli.
Bila shaka wamebarikiwa wale
waliokuona kwa macho wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi.
Ndiyo huyo Eliya aliyefunikwa
kwa kisulisuli; hata na Elisha naye akajazwa roho yake; akazidisha ishara
maradufu, na yale yaliyotoka kinywani mwake yalikuwa ya ajabu. Siku zake zote
huyu pia hakushawishwa kwa kumwogopa mwenye kutawala, wala hakutiishwa na mtu
yeyote. Hakutokea neno lililokuwa gumu la kumshinda, hata na alipolala mautini
mwili wake ulitoa unabii; kama alivyofanya miujiza katika maisha yake,
kadhalika na mauti yake kazi zake zikawa za ajabu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 97: 1 – 7 (K) 12
(K) Enyi wenye haki, mfurahieni
Bwana.
Bwana ametamalaki, nchi na
ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa
kiti chake. (K)
Moto hutangulia mbele zake,
Nao huwateketeza watesi wake
pande zote.
Umeme wake uliangaza ulimwengu,
Nchi ikaona ikatetemeka. (K)
Milima iliyeyuka kama nta mbele
za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu
wake. (K)
Na waaibishwe wote waabuduo
sanamu,
Wajivunao kwa vitu visivyofaa;
Enyi miungu yote, msujuduni
Yeye. (K)
SHANGILIO
1 Sam. 3:9
Aleluya, aleluya,
Nena Bwana, kwa kuwa mtumishi
wako anasikia, Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
INJILI
Mt. 6:7-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake:
Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani
ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao;
maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.
Basi ninyi salini hivi; Baba
yetu uliyembinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako
yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe
deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni,
lakini utuokoe na yule mwovu.
Kwa maana mkiwasamehe watu
makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu
makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2026, "MASOMO
YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings
reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:
Post a Comment