Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MEI 24, 2024



MASOMO YA MISA, MEI 24, 2024
IJUMAA, JUMA LA 7 LA MWAKA


SOMO 1
Yak. 5:9-12

Ndugu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.
Lakini Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103: 1-4, 8-9, 11-12 (K) 8

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu 
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, 
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)

Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)

Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta siku zote,
Wala hatashika hasira yake milele. (K)

Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali ya magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)


SHANGILIO
1 Kor. 5:19

Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.


INJILI
Mk. 10:1-12

Yesu alifika mipakani mwa Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hata ya talaka na kumwacha.

Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo. 


Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment