MASOMO YA MISA, MEI 22, 2024
JUMATANO, JUMA LA 7 LA MWAKA
SOMO 1
Yak. 4: 13-17
Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji Fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida; walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kasha hutoweka. Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi. Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya. Basi yeye naye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 49: 1-2, 5-10 (K) Mt. 5:3
(K) Heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Sikieni haya, enyi mataifa yote;
Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani.
Watu wakuu na watu wadogo wote pia,
Tajiri na maskini wote pamoja. (K)
Kwa nini niogope siku za uovu,
Ubaya ukinizunguka miguuni pangu?
Wa hao wanaozitumainia mali zao,
Na kujisifia wingi wa utajiri wao. (K)
Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake,
Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake.
Maana fidia ya nafsi zao ina gharama,
Wala hana budi kuiacha hata milele
Ili aishi siku zote asilione kaburi. (K)
Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa;
Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja,
Na kuwaachia wengine mali zao. (K)
SHANGILIO
2Tim. 1:10
Aleluya, aleluya,
Mwokozi wetu Yesu Kristo, alibatili mauti na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili.
Aleluya.
INJILI
MK. 9:38-40
Yohane alimjibu Yesu akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment