MASOMO YA MISA, JUMAPILI MEI 26, 2024
SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU
JUMAPILI BAADA YA PENTEKOSTE - MWAKA B
SOMO 1
Kum. 4 :32-34, 39-40
Musa aliwaambia makutano: Uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? Je! watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife? Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile Bwana, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu?
Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa Bwana ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo Bwana, Mungu wako, milele.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 33 :4-6, 9, 18-20, 22 (K) 13
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
Kwa kuwa neno la Bwana ni adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Bwana huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika.
Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake.
Maana Yeye alisema, ikawa;
Na Yeye aliamuru, ikasimama. (K)
Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
Nafsi zetu zinamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)
SOMO 2
Rum. 8 :14-17
Kila mtu anaongozwa na Roho wa Mungu, huyo ndio mtoto wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithi pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
SHANGILIO
Ufu 1:8
Aleluya, Aleluya,
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.
Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.
Aleluya.
INJILI
Mt. 28: 16-20
Wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda Galilaya mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu. Nao walipomwona, walimsujudia; lakini baadhi yao waliona shaka. Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi sikuzote, hata ukamilifu wa dahari.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment