“ASALI ITOKAYO MWMABANI”
Tafakari ya Pasaka
Alhamisi, Mei 31, 2023.
Juma la 8 la Pasaka
Sikukuu ya Maamkio ya Bikira Maria.
Rum 12: 9-16;
Is 12: 2-6;
Lk 1: 39-56.
MAMA MARIA TUTEMBELEE SISI!
Leo ni sherehe ya maamkio ya Bikira Maria alipoenda kumtembelea Elizabeti. Tendo hili tunalitaja kama tendo la furaha katika historia yetu ya wokovu kwenye rozari takatifu. Maria baada ya kupokea ujumbe mkubwa kabisa wa habari njema aliondoka kwenda kumshirikisha ujumbe huu wa furaha Elizabeti. Tofauti na siku nyingine ambazo Maria humtembelea, safari hii Maria anabaki ili kumsaidia, kwasababu alihitaji msaada. Alimjali kweli.
Kama Maria na Elizabeti, tunapaswa kushirikisha furaha yetu, huzuni yetu, kujali na kujitoa, kuwa na moyo mwema wakuweza kutoa maneno ya kufariji na kutia moyo wengine, maneno ya faraja, kumpa mtu hakika kwamba utamuombea nk, kwa wale walio katika matatizo na uchungu. Wanawake hawa wawili katika sikukuu ya leo ni mifano inayongara kwetu sisi wote. Na zaidi sana hasa kwenye ulimwengu huu ambapo wengi wamekuwa wabinafsi na hawataki kujali wengine wakidhani ndio muondoko mpya wa maisha ya kisasa. Kujijengea geti na kujificha ndani.
Kwa njia nyingine wimbo wa Bikira Maria, unaonesha hali ambayo tunapaswa kuwa nayo katika mioyo yetu. Tofauti na sisi, Bikira Maria, aliweka yote kwa Mungu. Inaonesha ni mara ngapi sala yake inamuelezea Mungu. Katika wimbo wake maneno kama, Mwenyezi, Bwana, Mungu, Mwokozi, Mtakatifu nk, yanaonesha kabisa maisha ya Maria yalikuwa ya Imani na sala na yalijikita kwa Mungu mwenyewe. Kadiri alivyofahamu ukuu wa Mungu ndivyo alivyojitambua hana kitu. Ni jinsi ghani itakuwa vyema kama tutajifunza kila siku jinsi ya kuondoa muonekano wetu wa uongo, na kuruhusu utu wa Kristu ukue ndani yetu.
Mama Maria ni Malkia wa wale wote wanao jitahidi kutafuta utakatifu. Anaendelea kuwatembelea wale wote walio na mahitaji ya pekee kila wakati. Tuna uwezo wa kujenga uhusiano naye ambao anauleta kwetu kwa huruma isiyo na mwisho kutoka kwa Mwanae. Uhusiano wa neema tunaoweza kuwa nao na Mama yetu ni uhusiano wa ndani kabisa tunaoweza kuwa nao kwa yeye kututembelea. Alimtembelea Elizabeth siku nyingi zilizopita na sasa anatamani kukutembelea kukuletea neema alizo nazo kutoka kwa Mwanae. Mkaribishe ndani, msikilize, kuwa wazi kwa neema anazo leta na furahia kama Elizabethi kwamba Mama wa Bwana wangu amenijilia mimi.
Sala: Mama Yangu mpendwa Maria, ninakupenda wewe na nakabidhi maisha yangu kwako, nikiamini msaada wako wa kimama na maombezi yako kutoka kwa Mwanao. Ninaomba niwe wazi niweze kupokea yote unayo niletea kutoka kwa Mwanao, Yesu Kristo. Nina heshimu na kunyenyekea kwamba utanijali mimi na natamani uniletee huruma ya Moyo wa Mwanao Yesu. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com
No comments:
Post a Comment