Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUONGEA LUGHA YA UPENDO



“MBEGU ZA UZIMA”
Tafakari ya Pasaka
Jumapili Mei 5, 2024
------------------------------------------------
DOMINIKA YA 6 YA PASAKA 

Somo la 1: Mdo 10: 25-26, 34-35, 44-48 Tunasikia kufunguliwa kwa jumuiya ya Wakristo kwa watu wa mataifa na jinsi Roho Mtakatifu anavyokuja juu ya umati waliokuwa na Petro. Kornelius, akida wa kirumi, anakuwa mpagani wa kwanza kupokea neema ya ubatizo. Mungu habagui katika upendo wake. Upendo wake ni kwa ajili ya wote. 

Wimbo wa katikati: Zab 98: 1-4 Mungu amedhihirisha wokovu wake kwa mataifa yote. 

Somo la 2: 1 Yn 4: 7-10 Yohane anatuambia kwamba tunapaswa kupendana sisi kwa sisi kwasababu Mungu ni Pendo. Mmoja hawezi kufahamu lolote kuhusu Mungu kama hajui upendo. 

Injili: Yn 15: 9-17 Yesu anaongea na marafiki zake usiku ule kabla ya kifo chake. Anawaacha na amri kuu “Pendaneni, kama mimi nilivyo wapenda ninyi”.
------------------------------------------------

KUONGEA LUGHA YA UPENDO

Kulikuwa na Bwana mmoja alikuwa akilima shamba lake na kupata mahindi mengi kweli kweli. Watu walishangaa ni mbinu gani anatumia ili kuzalisha mahindi mengi namna hii. Mwandishi mmoja wa habari akaamua kwenda kumuuliza yule bwana, hivi ni mbinu gani unatumia wewe kiasi ambacho wewe kila mwaka unalima mahindi lakini cha ajabu wengine wanaweza wakapata kidogo lakini wewe ukapata sana? Yule bwana akamwambia, kwakweli mimi kabla sijalima nahakikisha wale majirani zangu wote wanaonizunguka nawanunulia mbegu za mahindi yale yale ambayo nitayaotesha ili uchavushaji kwa njia ya wadudu kutoka katika mahindi yangu na mahindi yao yasije wakadumaza mahindi yangu. Hivyo nahakikisha tunaotesha mbegu zilizo fanana. Kwani wakiotesha mbegu ambazo hazifanani na za kwangu kwakweli zinatadumaza mahindi yangu.  Ooh kumbe, kwa tone lake la upendo kwa wale majirani linamfanya yeye apate mafanikio? Mwandishi akafahamu na kufurahia na kutambua siri ya mafanikio yake. 

Ndugu zangu mfano huu hapo juu unasisitiza juu ya amri ya mapendo ambayo Yesu anasisitizia katika Injili. Wakati tukiwa wabinafsi na kukataa kushirikisha kama Yesu anavyotuambia. Tukijijengea ukuta na kukataa kushirikishana na wengine, inakuwa kana kwamba tunakataa mafanikio yetu sisi wenyewe. Sisi wenyewe tunakuwa ndio wa kwanza kuanza kuteseka. Tunapo kuwa na kila kitu kwa ajili yetu wale wote walio karibu yetu wanahisi tu kama hali ya ukame inatoka kwetu, na moja kwa moja utaona wakitukimbia sisi.

Tunapo amua kuonesha upendo wa Kristo tunakuwa tunaangusha kuta zote za ubinafsi wetu na na kuleta hali ya kujali kama Yesu anavyosema. Tunajifungua wenyewe kwa Kristo. Na sisi wenyewe tunakuwa wa kwanza kufaidi. Tunakuwa tunafurahia matunda ya urafiki wetu kama huyu bwana alivyokuwa akifurahia kupata mahindi kila mwaka. Tunapata Amani, na katika hali hii tunakuwa na kuzaa matunda mema. Na watu wanafurahia na kushangilia kwa kile wanachopata kutoka kwetu. 

Kupendana sisi kwa sisi inadai pia ukomavu. Kwanza kabisa lazima tuone uhitaji wa mwingine kwetu. Kupenda nikujifungua kwa mwingine na kuwa tayari kukabili mahitaji yake. Kuwa na moyo wa kutokutarajia kupata kutoka kwao, kwani wengine wanachukua hata bila kutarajia kurudisha. Hii ina maana kwamba kuwa tayari kijiweka katika hatari kwasababu ya kupenda.

“Pendaneni ninyi kwa ninyi”, Yesu anasema “kama nilivyo wapenda ninyi” “kwa wale wanaoshika amri hii hawataona ukame kamwe. Katika jioni ya maisha yetu tutapokea hukumu ya upendo. (Mt. Yohane wa Msalaba). Katika somo la kwanza Kornelius, akida wa kirumi, anakuwa mpagani wa kwanza kupokea neema ya ubatizo. Hapa Mungu anadhihirisha upendo wake kwa wote. Mungu habagui katika upendo wake. Upendo wake ni kwa ajili ya wote, sio kwa Wayahudi peke yao bali kwa wote waliotayari kumpokea, huwajalia kuwa watoto wake kwa mapendo makuu. Na katika somo la Pili Yohane naye anatuamuru pia nasi tupendane kwani Mungu ni Upendo, hakuna njia nyingine ya kuonesha kwamba sisi ni watoto wa Mungu kama hatupendani. Katika pendo tutawavuta wengi kwa Kristo. 

Sala: Ee Bwana ninakuaomba nijifunze lugha yako ya upendo. Ninakuomba niongee na wote ninaokutana nao na wote wanaonizunguka. Ninakuomba niweze kuwa mkristo mwenye marafiki wengi iwezekanavyo wanaokupenda na kujazwa furaha na upendo. Amina

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment