Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

WAHUJAJI WA KUELEKEA MBINGUNI!


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
JUMAPILI, Mei 12, 2024. 
Juma la 7 la Pasaka

Mdo 1:15-17, 20-26
1 Yn 4:11-16
Yn 17:11-19


WAHUJAJI WA KUELEKEA MBINGUNI!

Siku moja Mfalme mmoja alitaka kufanya sherehe. Akaamua kuwaambia wafanyakazi wake kila mtu alete chupa moja ya divai ili kila mtu akileta tuweke kwa pamoja kwenye dumu moja kubwa kwa pamoja na tuanze sherehe yetu. Na hicho kitakuwa kinywaji chetu wote. Mzee mmoja akafikiri moyoni kwamba mimi nina chupa ya kuwekea divai na hata nikiweka maji hayawezi kuonesha kama maji watu wataona kama nimebeba divai. Hivyo nitaenda mwenyewe nimimine  kwenye dumu kubwa mwenyewe kwani nani ataniona kama nimeweka maji? Akasema nitafanya kwa siri na wala hakuna mtu ataniona kwani chupa moja tu ya maji kati ya chupa zote nyingi za divai wengine watakazoleta hata mtu akionja hatagundua hilo. Kumbe cha ajabu wazo hili la huyu mzee halikuwa wazo lake mwenyewe kumbe na wengine karibu wote waliwaza kama yeye. Siku ya sherehe wakaleta maji wote. Na mmoja tu ndiye alieleta divai, hivyo wakakosa divai ya sherehe. 

Ndugu zangu katika somo la Injili Yesu anawaombea wanafunzi wake umoja anataka wafanye kazi kwa ushirikiano kila mtu akijitoa bila kutegea. Mfano huo utufundishe sisi wenyewe jinsi ya kujitoa kwa ajili ya umoja wa kanisa, kila mmoja awaze kuleta mafanikio mazuri katika kanisa la Mungu. Kila afanyacho kilenge katika kujenga Umoja na utume wa kumtangaza Kristo. Lakini Pia Yesu anaomba Baba atuweke katika ile kweli ili tuweze kutenda katika kweli. Hivyo katika utume wetu tutende katika kweli tusilete maji, bali matunda mema-divai njema kwa ajili ya furaha ambayo Mungu ametualika katika sherehe ya Mbinguni. Wote tumealikwa tupeleke divai Mbinguni, divai ya matendo mema naya utume wa Ukristo wetu, tusipeleke maji. 

Bwana alishapaa na sasa anajiandaa kutupelekea Roho Mtakatifu juu yetu. Tunapaswa kuwa na mioyo iliyofunguka ili kutulepekea nguvu hii ya Roho Mtakatifu. Tunapaswa kuwa na mioyo inayoamini kwa ndani kabisa kwa Yesu Kristo na Kanisa lake Takatifu. Tunataka kufanywa upya kabisa ili utukufu wa Mungu uweze kuonekana katika ulimwengu. 

Somo la kwanza leo ni kutoka katika Matendo ya Mitume. Mitume wa Yesu sasa wanamweka mtume mwingine badala ya Yuda yule ambaye alimsaliti Yesu. Kuna hali ya kufikiri kwamba mitume wa Yesu lazima wabaki kumi na mbili na hivyo Yuda Iskariote ambaye hayupo sasa lazima waweke mtu badala yake. Baadaye kundi hili linakuwa maaskofu wa kanisa. Na baadae sio tena kumi na mbili bali wale wote wanaoshiriki katika hali ile ile ya mitume. Kwa kuwa wachungaji wa kila kundi katika sehemu mbali mbali za dunia. 

Somo la pili leo ni kutoka katika barua ya kwanza ya Yohane. Haipaswi kutushangaza kabisa kwamba katika barua hii Yohane anatuambia tunapaswa kuendana sisi kwa sisi. Yohane anatuambia kama tukipendana sisi kwa sisi Mungu anakuwa kati yetu na anafanya upendo uwe katika ukakamilifu”. Kama tukipendana….. hii ndio maada kuu. Pendaneni. Tunajuaje kwamba tunapendana. Kwasababu ametupatia sisi Roho wake Mtakatifu. Na hii ndio maana tunasubiri kwa furaha siku ya Pentekoste. Tunataka kusheherekea tena kwamba Yesu ametupatia Roho Mtakatifu na hivyo tuna nguvu ya kupendana sisi kwa sisi. 

Yesu ujumbe wa upendo tayari alishaunza na Yohane aliulewa vizuri sana ndio maana anaundika katika somo la pili. Katika Injili Yesu anawaombea mitume wake wabaki wamoja kama vile yeye na Baba walivyo wamoja. Yesu anatutaka sisi tuwe wamoja sisi kwa sisi kama vile yeye mwenyewe alivyo mmoja na Baba. Inaonekana kuwa ya kipekee, lakini katika hali ya kweli kuna watu wengine tukiwaangalia hatuna uhakika kama tunaweza kuwa wamoja pamoja nao. Ubinadamu wetu unatusukuma sisi tusiwakaribishe katika maisha yetu. Tunachagua ubinadamu wetu zaidi na tunakataa kuchagua hali ya Kimungu.

Mara nyingi tunashindwa kuwapenda wenzetu kwasababu tumeshaweka mawazo mabayo juu yao katika akili zetu. Na hivyo tunashindwa kuwapenda kwani tayari tumesha wahukumu. Tuondoe hukumu iliopo ndani ya vichwa vyetu kuhusu wengine ili tuweze kufungua mlango wa upendo kwa wote bila kuwatenga. 

Pengine wakati mwingine tunashindwa kuwapenda wengine kwasababu ya makosa ambayo walishatenda. Tunaona kana kwamba hawana tena nafasi katika maisha yetu. Ebu fikiria Petro alivyomkana Yesu lakini bado Yesu anamuamini na kumkabidhi Kanisa? Tuache kuwafungia watu kwenye box, tutashindwa kuwapenda. 

Sala ya pamoja ina nguvu sana katika kuwaweka watu katika umoja. Yesu anawaombea wabaki katika umoja. Katika hali ya kweli matatizo mengi tulionayo kwenye familia zetu, ukosefu wa Amani, na magomvi ni kwasababu hatusali. Hatuna muda wa kusali pamoja kifamilia. Wakati wa sala hata hasira ya mama au baba yaweza kuondoka na Amani kurudi. Mara nyingi tunapatwa na matatizo kwasababu pengine hatusali na tunajitegemea wenyewe. Hata shetani anaogopa sala ya pamoja. Anajua akija akiwakuta wote hawezi kuwashinda. Ukiwa mwenyewe ni rahisi sana shetani kukushinda. Sali na wenzako ili Bwana awe katikati yetu, kama alivyo ahidi. Walipo wawili au zaidi kwa ajili yangu nipo katikati yao. Tuoneshe upendo na umoja katika sala na hili linawezekana kama tutamkaribisha Roho Mtakatifu.  

Ni Roho wa Mungu anaweza kutufanya sisi viumbe vipya na kutufanya sisi tuwe wamoja. Ni pale tu tunapo chagua kuishi ndani ya Roho Mtakatifu sisi wote tutakuwa wamoja kwani atatufundisha yale yote ya Kristo. Yeye ndiye atatuongoza katika njia ya kweli na kutenda yale yanaompendeza Mungu. Tuombe neema hiyo ya Umoja katika Novena yetu pia. Tumsifu Yesu Kristo.

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

1 comment:

  1. This Sunday is Ascension of Jesus and the reflection is of 7th Sunday of Easter. Those who maintain this website should be more serious and not just work for the sake of doing it. Kindly be more true to the work.

    ReplyDelete