Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MUNGU ASIYE JULIKANA!


“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya Pasaka
Jumatano, Mei 8, 2024 
Juma la 6 la Pasaka

Mdo 17: 15, 22-18:1;
Zab 148: 1-2,11-14;
Yn 16:12-15.

MUNGU ASIYE JULIKANA!

Katika somo la kwanza, Mt. Paulo anawavuta watu wa Atheni katika utambuzi kuhusu altare zao walizojenga kwa “Mungu asiye julikana”. Anawaeleza kwamba amekuja kuwafunulia ukweli juu ya huyu Mungu asiye julikana wanaye mwabudu waweze kumtambua yeye ni nani. Wakati mwingine tunamtazamia Mungu ambaye tunataka kumuona au kumshika. Wakati mwingine tunajikuta tunakimbilia mara nyingi sehemu ambazo tunaona Mungu amechorwa katika picha ya kibinadamu. Lakini tunapaswa kutambua kwamba Mungu wetu ni Mungu aliyefichika (Is 45: 15). Amefichika katika ufahamu wetu. Katika wimbo wa kuabudu tunaimba ‘Yafichika machoni Imani yaona’, fahamu haiwezi kutambua fumbo hili bali Imani inatusaidia.

Katika Injili Yesu anatufunulia kuhusu Utatu Mtakatifu. “Roho atakayekuja atachukua kila kilicho changu” (Yn 16:14). “kila alicho nacho Baba ni changu” (Yn 16: 15). Hapa umoja wa Utatu Mtakatifu na asili ya nafsi tatu unafunuliwa.

Hii inamaana kwamba tunapaswa kuwa wazi katika maisha yetu juu ya nguvu na uwepo wa Roho Mtakatifu, yeye aliyebeba ukweli wote. Roho Mtakatifu anapaswa kuwa hai ndani mwetu, akifunua ukweli. Na tukiwa wazi kiakili na mioyo yetu kwa Roho Mtakatifu, tutakuwa watu wakutamani ukweli. Tutakuwa na hamu ya kuelewa vitu ambavyo vitafungua mioyo yetu. Tutakuwa na uwezo wakutazama mambo katika hali ya upya. 

Wewe ni wazi kiasi ghani katika uweli? Ni mara ngapi katika hali ya kweli unakumbatia yote ambayo Mungu ameyafunua kwako? Jifungue zaidi kwa Roho Mtakatifu na tafuta yote ambayo anayafunua kwako. 

Sala: Roho Mtakatifu, ninaomba uje utawale maisha yangu. Nifundishe na kuniongoza katika ukweli wote. Roho Mtakatifu, Bwana Mtakatifu, Baba mwenyewe huruma, nakuamini wewe. Amina.

Copyright ©2013-2024 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com

No comments:

Post a Comment