Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

SIKU YA TISA: JUMAMOSI BAADA YA PASAKA


SIKU YA TISA: JUMAMOSI BAADA YA PASAKA


NAMNA YA KUFANYA NOVENA KWA HURUMA YA MUNGU

Sala ya kutubu:
Mungu wangu, ninatubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi, basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi kwako, Amina.

Nia ya sala za leo:
SIKU YA TISA

Maneno ya Mwokozi wetu: “Leo niletee roho za wale waliokwishaingia hali ya uvuguvugu, na uwazamishe katika kilindi cha Huruma yangu. Roho hizi huumiza sana Moyo wangu. Roho yangu iliteseka sana kwa kinyaa cha kutisha kule bustanini kwa sababu ya roho hizi vuguvugu. Ni wao waliosababisha nilie; Baba ikiwa ni mapenzi yako uniondolee mbali kikombe hiki nisikinywe. Kwa watu hawa, tumaini la mwisho lililowabakia ni kuikimbilia Huruma yangu tu basi”.

Tuwaombee watu walio na hali ya uvuguvugu, hali ya hatari kwa wokovu, ambao walisababisha mateso makali sana kwa Yesu Kristu kule bustanini mwa mizeituni.

W: Ee Yesu mwenye Huruma nyingi, Wewe u Huruma yenyewe, Uzipokee roho vuguvugu ndani ya Moyo wako ulio na Huruma bila kiasi. Roho hizi ni kama mizoga iliyojaa na kunuka uvundo, uziingize katika moto wa upendo wako safi, zitakasike. Roho hizi zilikutia kinyaa kingi. Sasa uziwashe tena, na kwa Huruma yako, uzipe paji la Upendo Mtakatifu. Ee Yesu mwenye Huruma Kuu, tumia uwezo wako na uzipatie roho hizi bidii tena, kwani kwako hakuna kitu kisichowezekana, na kwa njia hii wapate kuitukuza daima Huruma Yako. Amina.

Baba yetu,       Salamu Maria ………..Atukuzwe,       

W: Baba wa Huruma, uzitazame kwa macho ya Huruma, roho zilizo vuguvugu, ambazo katika hali yao hiyo, wameingizwa ndani ya Moyo wa Mwanao Yesu, ulio kilindi cha Huruma. Ee Baba wa Huruma, tunakusihi kwa ajili ya mateso makali ya Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristu, uliyovumilia pale msalabani, kwa masaa matatu ukiwa katika hali ya umahututi ya uchungu, uziwezeshe hata roho hizi zipupie utukufu wako. Uijaze mioyo ya watu hawa upendo wa kweli, hivyo kwa Baraka takatifu, waweze kutenda matendo mengi ya huruma hapa duniani, na huko Mbinguni wafike kuitukuza Huruma yako Kuu kwa milele yote. Amina.

Rozari  ya Huruma ya Mungu
(Tumia chembe za rozari ya kawaida)
Baba yetu …       Salamu Maria …. x3            Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi …….

Kwenye chembe kubwa
Baba wa Milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu, wa Mwanao Mpenzi sana, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zetu, na dhambi za dunia nzima.

kwenye chembe ndogo
Mwanzishaji: Kwa ajili ya mateso makali ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Wote huitika: Utuhurumie sisi na dunia nzima.

Mwisho wa Rozari sali mara tatu sala ifuatayo:
Mungu Mtakatifu, Mtakatifu mwenye Enzi, Mtakatifu unayeishi milele, Utuhurumie sisi na dunia nzima.


Litania ya Huruma ya Mungu


No comments:

Post a Comment