Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

NOVENA YA HURUMA YA MUNGU SIKU YA SABA: ALHAMISI BAADA YA PASAKA




NOVENA YA HURUMA YA MUNGU
SIKU YA SABA: ALHAMISI BAADA YA PASAKA


NAMNA YA KUFANYA NOVENA KWA HURUMA YA MUNGU

Sala ya kutubu:
Mungu wangu, ninatubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi, basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi kwako, Amina.

Nia ya sala za leo:
SIKU YA SABA

Maneno ya Mwokozi wetu: “Leo niletee roho za wale ambao kwa namna ya pekee huiheshimu na kuitukuza Huruma yangu, na uwazamishe ndani ya Huruma Yangu. Roho hizi ndizo zilizonisikitikia zaidi wakati wa mateso yangu na kuipenya kabisa roho yangu. Hawa ndio vielelezo na sura halisi ya Moyo wangu wenye Huruma na Wema. Roho hizi zitakuja kung’aa kwa namna ya pekee katika maisha ya milele ijayo. Hakuna hata mmoja kati yao atakayetupwa katika moto wa milele. Mimi Mwenyewe nitamkinga kwa namna ya pekee kila mmoja wao saa ile ya kufa kwao.”

Tuziombee roho za wale wanaoiheshimu kwa namna ya pekee Huruma ya Mungu, na kwa njia hii huwa sura hai za Moyo wa Yesu ulio na Huruma nyingi.

W. Ee Yesu mwenye Huruma, mwenye Moyo ulio Huruma yenyewe, uzipokee ndani ya Moyo wako wenye Huruma sana, roho za watu wale wanaoiheshimu na kuitukuza kwa namna ya pekee Ukuu wa Huruma yako. Roho hizi hushinda kwa nguvu ya Mungu mwenyewe. Hukazana kihodari, hata katikati ya taabu na dhiki za kila aina, wakiitumainia tu Huruma Yako, na kwa kujiunga nawe, ee Yesu, huwabeba wanadamu wote mabegani mwako. Watu hawa hutamani kushiriki Msalaba wako kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Uzidi kuwafunika kwa Huruma yako daima na uwajalie fadhila za uvumilivu, udumifu na nguvu za kuyasubiri yote. Amina.

Baba yetu,……. Salamu Maria …….. Atukuzwe, ………..

W. Baba wa Milele, uzitazame kwa macho ya Huruma, roho wa watu wale ambao kwa juhudi na upendo wa pekee, huitukuza na kuiheshimu Huruma yako isiyo na mipaka, ambao wameingizwa ndani ya Moyo wa Yesu ulio na Huruma tele. Watu hawa ni kama Injili iliyo hai. Wanakutukuza kwa maneno na matendo yao, na kwa kukuiga Wewe, huwatendea watu wenzao kwa wema na huruma. Tunakuomba uwaonyeshe Huruma yako Kuu zaidi na zaidi, kadri ya tumaini lao kwako na kwa ahadi zako. Mwanao Yesu Kristu Mwenyewe atawaleta kama utukufu wake, tangu wakati huu wakiwa bado hapa duniani. Lakini hasa saa yao ya kufa. Amina.

Rozari  ya Huruma ya Mungu
(Tumia chembe za rozari ya kawaida)
Baba yetu …       Salamu Maria …. x3            Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi …….

Kwenye chembe kubwa
Baba wa Milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu, wa Mwanao Mpenzi sana, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zetu, na dhambi za dunia nzima.

kwenye chembe ndogo
Mwanzishaji: Kwa ajili ya mateso makali ya Bwana wetu Yesu Kristo,
Wote huitika: Utuhurumie sisi na dunia nzima.

Mwisho wa Rozari sali mara tatu sala ifuatayo:
Mungu Mtakatifu, Mtakatifu mwenye Enzi, Mtakatifu unayeishi milele, Utuhurumie sisi na dunia nzima.


Litania ya Huruma ya Mungu

No comments:

Post a Comment