Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATATU, JANUARI 8, 2024


MASOMO YA MISA, JUMATATU, JANUARI 8, 2024
SHEREHE YA UBATIZO WA BWANA


MWANZO:
Mat. 3:16-17

Bwana alipokwisha kubatizwa, mbingu zikamfunukia, Roho akashuka kwa mfano wa hua, na kukaa juu yake; na tazama, sauti ya Baba ikasema: Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.


SOMO 1
Isa. 42:1-4, 6-7

Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 29:1-4, 9-10 (K) 11

(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu. (K)

Sauti ya Bwana I juu maji
Bwana yu juu ya maji mengi
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina adhama. (K)

Sauti ya Bwana yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)


SOMO 2
Mdo. 10:34-38

Siku ile: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa nay eye.

Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli, akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
Mk. 9:7

Aleluya, aleluya,
Mbingu zilimfunguka na sauti ya Baba ikasikilika,
“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”
Aleluya.


INJILI
Mk. 1:7-11

Siku ile: Yohane alihubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.

Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohane katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.

copyright © 2024, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment