MASOMO YA MISA, JANUARI 3, 2024
JUMATANO, KIPINDI CHA NOELI
SOMO 1
1 Yn. 2:29 – 3:6
WAPENZI: Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa nay eye. Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu. Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi, kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1, 3-6 (K) 36
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu,
Mshangilieni Bwana nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO
Ebr. 1:1-2
Aleluya, aleluya,
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi na kw anamna nyingi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.
INJILI
Yn. 1:29-34
Siku ile, Yohane alimwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu; ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji.
Tena Yohane akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye Akaka juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment