Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUFANYA MIOYO YETU KUWA SEHEMU YA MUNGU KUKAA


MBEGU ZA UZIMA”
Desemba 24, 2023
DOMINIKA YA 4 YA MAJILIO

------------------------------------------------
Somo la 1: 2 Sam 7: 1-5, 8-12, 14, 16 mfalme Daudi anataka kujenga hekalu kwa ajili ya Mungu. Lakini Mungu anamwambia, Yeye mwenyewe ndiye atakaye jenga nyumba na ufalme wake utadumu milele. 

Wimbo wa Katikati Zab 88: 2-5, 27, 29 Mungu amefanya Agano na wateule wake, na ataweka upendo wake nasi daima, tukiwa naye Agano letu litadumu. Na tutaimba milele juu ya upendo wake. 

Somo la 2: Rom 16: 25-27 mpango wa Mungu wa ukombozi kwa Wayahudi na watu wa mataifa unatimilika kwa njia ya Kristo. Habari njema sasa inapaswa kudhihirishwa na kutangazwa kila mahali.

Injilil: Lk 1: 26-38 Tunasikia jinsi Mungu anavyo ongea na Maria kwamba atakuwa Mama wa Mwanae na Mama Maria anautoa utashi wake na kukubali kuwa Mama wa Mkombozi. Ingawaje hakuwa ameelewa bado vizuri.
------------------------------------------------

KUFANYA MIOYO YETU KUWA SEHEMU YA MUNGU KUKAA 

Majilio inaisha na Noeli ipo mlangoni inagonga. Masiha ambaye tulikuwa tukimsubiria yupo mlangoni anabisha hodi katika maisha yetu. Tangu Mwanadamu alipo jitenga na Mungu kwa njia ya dhambi, Mungu anatangaza uamuzi wake wakuja yeye mwenyewe. Mpango wa kumvuta mwanadamu kwake tena. Na kwakumleta Yesu duniani alihitaji mama, hekalu takatifu atakamo kaa Mwanae. 

Masomo yetu yote leo, somo la kwanza na injili yanaongelea nyumba. Katika somo la kwanza, Daudi yupo nyumbani kwake anakaa chini anafikiria kumjengea Mungu nyumba. Mungu anaelewa hamu ya Daudi, lakini yeye mwenyewe anajitokeza na kutangaza mpango wake wa kuanzisha familia yake ya milele. Baada ya kifo cha Daudi, mtoto wake Solomoni alichukuwa nafasi yake na alijenga hekalu zuri kwa ajili ya Mungu. Alitawala zaidi ya miaka arobani, lakini ufalme wake uliisha. Na kwa njia hii Wayahudi walikuwa wanauliza, “Kimetokea nini kuhusu ahadi ya Mungu kwa Daudi, kwamba Ufalme wake utadumu milele? Je, Mungu ameshindwa kutimiza ahadi yake? Jibu lao lipo katika somo la Injili kwamba Mungu hakushindwa katika ahadi zake. Ili kutimiza ahadi yake alimchagua msichana mdogo tena mnyenyekevu, Maria. Alikuwa hekalu la Mungu ambamo atakaa. Kwa miezi tisa aliishi ndani yake kama hekalu. Maria amekuwa Agano jipya, ambapo Mungu ameishi kati ya watu. Baada ya kufahamu mpango wa Mungu, Maria alijitoa bila kujibakiza kwa ajili ya mpango huo. “Mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyo nena” (Lk. 1:38) 

Kitu kingine cha kuangalia ni kuhusu kulinganisha Daudi na Maria. Daudi anataka kufanya kitu kikubwa kwa ajili ya Mungu, na Maria anaonesha hamu yake ya kupokea kitu kikubwa kutoka kwa Mungu, Mwanae wa pekee. Njia aliyotumia Maria ndiyo njia ambayo Mungu anaipenda. Mungu alimuulizia Maria kwa ajili ya nyumba ambayo Mwana wake atakaa, naye alitoa mwili wake. Kwake ulikuwa ni ukarimu wa hali ya juu. Kwake Mungu alipata hekalu na nyumba ya kukaa ndani yake. Kwa njia yake Mwanae alikuja ulimwenguni na kubadili maisha ya watu. 

Wakati tukiwapatia watu wengine zawadi za Noeli, tutambue pia Mungu ametupatia sisi jua, mwezi na nyota, dunia nzima misitu milima na bahari na vyote viijazavyo. Anatupatia sisi vitu vyote na vyote vivumavyo na kuzalisha matunda-hata vile ambavyo tunapigania na ambavyo tumetumia vibaya. Na ili kutukomboa kutuokoa katika hali ya dhambi zetu, amemtuma Mwanae ulimwenguni. 

Wakati mmoja anapo pokea zawadi anakiri uwepo wakumshirikisha mwingine katika maisha yake. Leo, tunasubiria ujio wa Kristo kesho. Lakini pia Yesu anasubiri “ndiyo” yetu, kama alivyo isubiri kutoka kwa Maria. Zawadi inakuwa ni zawadi tu pale inapo pokelewa. Je, sisi tupo tayari kupokea, kujikabidhi kwake, umaskini wetu na mioyo yetu? 

Njia pekee ya kuonesha kwamba tumemkubali ni kuwa wazi na kuwakaribisha wengine-kwa yeyote hasa kwa maskini na walio wapweke. Kuna mfano mmoja, kijana mmoja alikuwa anaitwa Martin, aliota kwamba Yesu atakuja kumtembelea. Siku zote alisubiria na kuendelea na shughuli zake. Katika kusubiria akawa amewapa baadhi ya maskini chakula, akawapa nguo baadhi ya maskini waliokuwa katika hali mbaya, mwingine alikuwa amemkosea akamsamehe. Siku nyingine akapatwa tena na ndoto, akaona Yesu anamuuliza, Je, Martini uliona nilivyokuja akasema hapana. Akamwambia nilikuja kwa njia ya wale uliowasaidia-yeyote uliowatendea walio wadogo hawa umenitendea mimi. Sio siku ya Krismasi tu Yesu anakuja na kubisha hodi katika mioyo yetu, anakuja kila siku na katika kila mwaka kwa ndugu zetu wote. 

Neno alifanyika mwili akakaa kwetu. Huu ni ujumbe uliojificha kwa miaka mingi lakini sasa umefunuliwa na kufanywa ujulikane kwa watu wa amataifa yote ili waamini na kutii. Mungu amekuwa akitimiza kazi yake ya ukombozi tangu miaka mingi. Katika kipindi hiki cha Noeli tumruhusu atukomboe. Noeli inavyo karibia tukuwe katika Imani na upendo tuweze kusheherekea.
.
Sala: Bwana, kipindi cha Noeli kinavyokaribia kabisa tunakuomba tuweze kukuwa katika Imani na kusheherekea ujio wa Kristo, ambaye ni Bwana milele na milele. Yesu anakuamini wewe. Amina

Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment