MASOMO YA MISA, NOVEMBA
5, 2023
DOMINIKA YA 31 YA MWAKA
A
MWANZO:
Zab. 38:21-22
Wewe Bwana usiniache,
Mungu wangu, usijitenge nami, ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana, wokovu wangu.
_____________
SOMO 1
Mal. 1:14 – 2:8-10
Kwa maana mimi ni Mfalme
mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa. Na sasa,
enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki
kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema Bwana wa majeshi, basi
nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani Baraka zenu. Bali ninyi mmegeuka
mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi,
asema Bwana wa majeshi. Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu
cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika
njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria.
Je! Sisi sote hatuna
Baba mmoja? Mungu aliyeumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu
anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?
Neno la Bwana…
_____________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 131
(K) Ee Bwana, uilinde
nafsi yangu katika amani yako.
Bwana, moyo wangu hauna
kiburi,
Wala macho yangu
hayainuki.
Wala sijishughulishi na
mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo
nguvu zangu. (K)
Hakika nimeituliza nafsi
yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto
aliyeachishwa,
Kifuani mwa mama yake,
Ndivyo roho yangu ilivyo
kwangu. (K)
Ee Israeli, umtumainie
Bwana,
Tangu leo na hata
milele. (K)
_____________
SOMO 2
1Thes. 2:7 – 9, 13
Kama vile mlezi
awatunzavyo watoto wake mwenyewe, vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo
mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia,
kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Maaana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na
masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu
wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu. Kwa sababu hiyo sisi
nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlilipokea lile neno la ujumbe la
Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno
la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi
mnaoamini.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
_____________
INJILI
Yn. 6:63, 68
Aleluya, aleluya,
Bwana maneno yako ni
roho, tena ni uzima, wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.
_____________
INJILI
Mt. 23:1-12
Yesu aliwaambia makutano
na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha
Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa
matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo
mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole
chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupaua
hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na
kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu,
Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni
ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye
mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye
Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza,
atadhiliwa; na yeyote atakayejidhili, atakwezwa.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
_____________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment