MASOMO YA MISA, NOVEMBA 20, 2023
JUMATATU, JUMA LA 33 LA MWAKA
SOMO 1
1Mak. 1:10-15, 41-43, 54-57, 62-64
Kulichipuka chipukizi chenye dhambi, ndiye Antioko Epifani, mwana wa mfalme Antioko, ambaye alikuwa amewekwa amana kwa Warumi. Naye alitawalishwa katika mwaka wa mia thelathini na saba wa enzi ya Wayunani.
Siku zile walitokea wahalifu sheria katika Israeli, wakashawishi wengi, wakisema, Twende tufanye maagano na mataifa wanaotuzunguka, maana tangu tulipofarakana nao misiba mingi imetupata. Jambo hilo likapendeza machoni pao, hata watu Fulani wakafanya hima kwenda kwa mfalme, naye akawapa ruhusa kuzifuata kawaida za mataifa. Wakafanya kiwanja cha michezo Yerusalemu kama kawaida ya mataifa, wakajifanya kana kwamba hawakutahiriwa wakajitenga na agano takatifu. Hivyo walijiunga na mataifa na kujiuza wafanye uovu.
Mfalme Antioko akaziandikia milki zake zote, kwamba wote wawe taifa moja, kila mtu aache sheria zake za asili. Watu wote wa mataifa wakaikubali amri ya mfalme, hata wengi katika Israeli walifuata ibada yake, wakitoa dhabihu kwa miungu ya uongo na kutia unajisi Sabato.
Siku ya ishirini na tano ya Kislevu, mwaka wa mia arobaini na tano, waliweka chukizo la uharibifu juu ya madhabahu, na katika miji ya Uyahudi kila upande walijenga vimadhabahu vya miungu, wakavukiza uvumba milangoni pa nyumba na njiani. Na vitabu vya sheria walivyovipata waliviparua vipande vipande wakaviteketeza. Mtu yeyote aliyepatikana na kitabu, au aliyeonekana anaifuata sheria, alihukumiwa kufa kama alivyoamuru mfalme.
Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile vitu vilivyo najisi. Waliona afadhali kufa kuliko kutiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano takatifu. Wakafa. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 119:53, 61, 134, 150, 155, 158 (K) 88
(K) Unihuishe kwa fadhili zako, nami nitazishika shuhuda za kinywa chako.
Ghadhabu imenishika kwa sababu ya wasio haki,
Waiachao sheria yako.
Kamba za wasio haki zimenifunga,
Sikuisahau sheria yako. (K)
Unikomboe na dhuluma ya mwanadamu,
Nipate kuyashika mausia yako.
Wanakaribia wanaonifuatia kwa chuki,
Wamekwenda mbali na sheria yako. (K)
Wokovu u mbali na wasio haki,
Kwa maana hawajifunzi amri zako.
Nimewaona watendao uhaini nikachukizwa,
Kwa sababu hawakulitii neno lako. (K)
SHANGILIO
Zab. 147:12, 15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
INJILI
Lk. 18:35-43
Yesu alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee mwana wa Daudi, unirehemu.
Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona. Akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu wote walipoona hayo walimsifu Mungu.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment