MASOMO YA MISA NOVEMBA 15, 2023
JUMATANO, JUMA LA 32 LA MWAKA
SOMO 1
Hek. 6:1-11
Enyi wafalme, sikilizeni; enyi waamuzi wa miisho ya dunia jifunzeni; sikieni ninyi mtawalao watu wengi, na kujisifia umati wa mataifa. Kwa maana mlipewa falme zenu na Bwana, na milki zenu na Aliye juu, ambaye atazichunguza kazi zenu, na kuyahojihoji mashauri yenu.
Kwa sababu, kisha kuwa wakuu wa ufalme wake, hamhukumu kwa adili, wala kuishika torati, wala kulifuata shauri la Mungu. Yeye atawajia ghafula kwa kitisho, madhali hukumu bila huruma huwaangukia wenye cheo; mradi mtu mnyonge aweza kusamehewa katika rehema, bali wakuu watadumhushiwa hasa. Kwa kuwa Bwana, Mfalme wa wote, hatajizuia kwa ajili ya mtu yeyote, wala hajali ukuu, kwa sababu ndiye Yeye aliyewafanya wadogo na wakuu pia. Naye huwazingatia watu wote pasipo upendeleo, walakini uchunguzi ulio halisi huwajilia wenye uwezo.
Kwa hiyo, enyi wafalme, nawaambia ninyi maneno yangu, ili mjifunze hekima, msije mkapotea njiani. Maana wale waliotunza kwa utakatifu mambo yale yaliyo matakatifu watahesabiwa kuwa watakatifu wenyewe; nao wale waliofundishwa hayo wataona neno la kujitetea. Basi fanyeni shauku ya maneno yangu; yatafuteni, na kwa malezi yake mtapata adabu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 82:3-4,6-7 (K) 8
(K) Ee Mungu, usimame, uihukumu nchi.
Mfanyieni hukumu maskini na yatima;
Mtendeeni haki aliyeonewa na fukara;
Mwokoeni maskini na mhitaji;
Mwopoeni mikoni mwa wadhalimu. (K)
Mimi nimesema, ndinyi miungu,
Na wana wa Aliye juu, nyote pia.
Lakini mtakufa kama wanadamu,
Mtaanguka kama mmoja wa wakuu. (K)
SHANGILIO
Zab. 119:34
Aleluya, aleluya,
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako, nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya.
INJILI
Lk. 17:11-19
Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, Yesu alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajioneshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.
Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, Imani yako imekuokoa.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment