MASOMO YA MISA NOVEMBA
10, 2023
IJUMAA, JUMA LA 31 LA
MWAKA
KUMBUKUMBU YA MT. LEO
MKUU (PAPA NA MWALIMU WA KANISA)
_____________
SOMO 1
Rum. 15:14-21
Ndugu zangu,
nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema,
mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri
zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba ninawakumbusha,, kwa neema ile
niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa,
niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye
kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu.
Basi, nina sababu ya
kuona fahari katika Kristo Yesu Mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno
asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa
tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata
ikawa tangu Yerusalemu, na kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili
ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri
hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi
wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake
wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
_____________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1-4 (K) 2
(K) Bwana ameufunua
wokovu wake.
Mwimbieni Bwana wimbo
mpya,
Kwa maana ametenda mambo
ya ajabu.
Mkono wa kuume wake
mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu
umemtenda wokovu. (K)
Bwana ameufunua wokovu
wake,
Machoni pa mataifa
ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema
zake,
Na uaminifu wake kwa
nyumba ya Israeli. (K)
Miisho yote ya dunia
imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi
yote,
Inueni sauti, imbeni kwa
furaha, imbeni zaburi. (K)
_____________
SHANGILIO
Yn. 14:5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema, mimi
ndimi njia, na ukweli, na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.
_____________
INJILI
Lk. 16:1-8
Yesu aliwaambia
wanafunzi wake: Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyekuwa na wakili wake; huyu
alishitakiwa kwake kuwa anatapanya mali zake. Akamwita, akamwambia, Ni habari
gani hii ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya uwakili wako, kwa kuwa huwezi kuwa
wakili tena. Yule wakili akasema moyoni mwake, Nifanyeje? Maana, bwana wangu
ananiondolea uwakili. Kulima, siwezi; kuomba, naona haya. Najua nitakalotenda,
ili nitakapotolewa katika uwakili, wanikaribishe nyumbani mwao.
Akawaita wadeni wa bwana
wake, kila mmoja; akamwambia wa kwanza, Wawiwani na bwana wangu? Akasema,
Vipimo mia vya mafuta. Akamwambia, Twaa hati yako, keti upesi, andika hamsini.
Kisha akamwambia mwingine, Na wewe wawiwani? Akasema, Makanda mia ya ngano.
Akamwambia, Twaa hati yako, andika themanini.
Yule bwana akamsifu
wakili dhalimu kwa vile alivyotenda kwa busara; kwa kuwa wana wa ulimwengu huu
katika kizazi chao wenyewe huwa na busara kuliko wana wa nuru.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristu.
_____________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment