MASOMO YA MISA, OKTOBA 6,
2023
IJUMAA, JUMA LA 26 LA
MWAKA
SOMO 1
Bar. 1:15-22
Kwa Bwana Mungu wetu,
haki; lakini kwetu sisi haya ya uso kama hivi leo, kwa watu wa Yuda na kwa
wenyeji wa Yerusalemu, na kw awafalme wetu, na kwa wakuu wetu, na kwa makuhani
wetu, na kwa manabii wetu, na kwa baba zetu, kwa sababu tumetenda dhambi mbele
ya Bwana. Tumemwasi, wala hatukuitii sauti ya Bwana Mungu wetu, kwenda katika
sheria zake alizoziweka mbele yetu. Tangu siku Bwana aliyowatoa baba zetu
katika nchi ya Misri hata leo tumemwasi Bwana Mungu wetu na kutenda yasiyofaa
kwa kutoisikiliza sauti yake.
Kwa hiyo mapigo haya
yameshikamana nasi, na ile laana ambayo Bwana alimwamuru mtumishi wake Musa,
katika siku aliyowaleta baba zetu kutoka katika nchi ya Misri ili atupe nchi
ijaayo maziwa na asali, kama hivi leo. Lakini hatukuisikiliza sauti ya Bwana Mungu
wetu, kwa kuyafuata maneno yote ya manabii aliyotupelekea, bali tulikwenda kila
mtu katika mawazo ya moyo wake mbaya, kutumikia miungu ya kigeni na kufanya
yaliyo maovu machoni pa Bwana Mungu wetu.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 79:1-6, 8-9 (K) 9
(K) Utusaidie, Ee Mungu,
kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Ee Mungu, mataifa
wameingia katika urithi wako,
Wamelinajisi hekalu lako
takatifu.
Wamefanya Yerusalemu
chungu chungu.
Wameziacha maiti za
watumishi wako
Ziwe chakula cha ndege
wa angani.
Na miili ya watauwa wako
Iwe chakula cha wanyama wa nchi. (K)
Wamemwaga damu yao kama
maji
Pande zote za
Yerusalemu,
Wala hapakuwa na mzishi.
Tumekuwa lawama kwa
jirani zetu,
Mzaha na dhihaka kwao
wanaotuzunguka.
Ee Bwana, hata lini? Utaona
hasira milele?
Wivu wako utawaka kama
moto? (K)
Usikumbuke juu yetu
maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije
kutulaki hima.
Kwa maana tumedhilika
sana. (K)
Ee Mungu wa wokovu wetu,
utusaidie,
Kwa ajili ya utukufu wa
jina lako.
Utuokoe, utughofiri
dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako.
(K)
________
SHANGILIO
Yn. 10:27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia
sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 10:13 – 16
Yesu aliwaambia wafuasi
wake: Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo
iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo,
huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu. Lakini, siku ya hukumu itakuwa
rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi. Nawe Kapernaumu,
je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu. Awasikilizaye ninyi
anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi
amkataa yeye aliyenituma.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment