MASOMO YA MISA OKTOBA
31, 2023
JUMANNE, JUMA LA 30 LA
MWAKA
_____________
SOMO 1
Rum. 8; 18-25
Nayahesabu mateso ya
wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule utakaofunuliwa kwetu. Kwa
maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa
Mungu. Kwa maana viumbe vyote pia vilitiishwa chini ya ubatili; si kwa hiari
yake, ila kwa sababu yake yeye aliyevitiisha katika tumaini; kwa kuwa viumbe
vyenyewe navyo vitawekwa huru na kutolewa katika utumwa wa uharibufu, hata
viingie katika uhuru wa utukufu wa watoto wa Mungu.
Kwa maana twajua ya kuwa
viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa. Wala si
hivyo tu; ila na sisi wenyewe tulio na malimbuko ya Roho, sisi pia tunaugua
katika nafsi zetu, tukikutazamia kufanywa wana, yaani, ukombozi wa mwili wetu.
Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana,
hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali
tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi.
Neno la Bwana…
Tumshukuru Mungu.
_____________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126 (K) 3
(K) Bwana alitutendea
mambo makuu.
Bwana alipowarejeza
mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao
ndoto.
Ndipo kinywa chetu
kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za
furaha. (K)
Ndipo waliposema katika
mataifa,
Bwana amewatendea mambo
makuu.
Bwana alitutendea mambo
makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)
Ee Bwana, uwarejeze watu
wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi,
Watavuna kwa kelele za
furaha. (K)
Ingawa mtu anakwenda
zake akilia,
Azichukuapo mbegu za
kupanda.
Hakika atarudi kwa
kelele za furaha,
Alichukuapo miganda yake.
(K)
_____________
SHANGILIO
Yak. 1:21
Aleluya, aleluya,
Pokeeni kwa upole neno
la Mungu lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya.
_____________
INJILI
Lk. 13:18-21
Yesu alisema, Ufalme wa
Mungu umefanana na nini? Nami niufananishe na nini? Umefanana na punji ya
haradali aliyotwaa mtu akaitupa katika shamba lake; ikamea, ikawa mti; ndege wa
angani wakakaa katika matawi yake.
Akasema mara ya pili,
Niufananishe na nini ufalme wa Mungu? Umefanana na chachu aliyotwaa mwanamke
akaisitiri ndani ya pichi tatu za unga, hata ukachacha wote pia.
Neno la Bwana… Sifa
kwako Ee Kristo.
_____________
Copyright © 2023,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment