Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA OKTOBA 26, 2023


MASOMO YA MISA OKTOBA 26, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 29 LA MWAKA

SOMO 1
Rum. 6:19-23

Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na hakim pate kutakaswa.

Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki. Ni faida gani basi mliyopata siku zile kwa mambo hayo mnayoyatahayarikia sasa? Kwa maana mwisho wa mambo hayo ni mauti. Lakini sasa mkiisha kuwekwa huru, na kuwa mbali na dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, mnayo faida yenu, ndiyo kutakaswa, na mwisho wake ni uzima wa milele. Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
_____________

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 1:1-4,6 (K) 40

(K) Heri aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.

Heri mtu yule asiyekwenda
Katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. (K)

Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)

Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushwayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
_____________

SHANGILIO
Yn. 15:15

Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
_____________

INJILI
Lk. 12:49-53

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi? Lakini nina ubatizo unipasao kubatiziwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!

Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katiak nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, nab inti na mamaye; mkwe na mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristu.

_____________

Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.


No comments:

Post a Comment