Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 28, 2023


MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 28, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 25 LA MWAKA

SOMO 1
Hag. 1:1-8

Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda na Yoshua, mwana wa Yeosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema, Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, watu hawa husema, hu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujengwa nyumba ya Bwana. Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema, Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika? Basi sasa. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; nay eye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka. Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu. Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
 ________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 149:1-6, 9 (K) 4

(K) Bwana awaridhia watu wake.

Aleluya,
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa!
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao! (K)

Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie!
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)

Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Na upanga mkali kuwili mikononi mwao. (K)

Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa:
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. (K)
 ________
SHANGILIO
Zab. 27:11

Aleluya, aleluya,
Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.
 ________
INJILI
Lk. 9:7 – 9

Herode mfalme alisikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohane amefufuka katika wafu, na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. Lakini Herode akasema, Yohane nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
________


Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment