MASOMO YA MISA, SEPTEMBA 22, 2025
JUMATATU, JUMA LA 25 LA MWAKA
SOMO 1
Ezr. 1:1-6
Ilikuwa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi,
mfalame wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia
lipate kutimizwa, Bwana akamwambia roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata
akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi: Bwana
Mungu wa mbinguni amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba
katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu
wake, Mungu wake na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda,
akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko
Yerusalemu. Na mtu awaye yote aliyesalia mahali popote akaapo hali ya ugeni, na
asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi
ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko
Yerusalemu.
Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa
Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu
amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya Bwana, iliyoko Yerusalemu.
Na watu wote, waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa
vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani,
zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 126 (K) 3
(K) Bwana alitutendea mambo makuu.
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.
Ndipo waliposema katika mataifa,
“Bwana amewatendea mambo makuu”. (K)
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi.
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini. (K)
Wapandao kwa machozi
Watavuna kwa kelele za furaha.
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda,
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
________
SHANGILIO
Yak. 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi
kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.
________
INJILI
Lk. 8:16 – 18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu
ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka uvunguni, bali
huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna
neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo
halitajulikana na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa
mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho
anadhaniwa kuwa nacho.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo
________
Copyright © 2025,
"MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora –
Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see
www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:
Post a Comment