Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATANO, AGOSTI 5, 2026




MASOMO YA MISA, JUMATANO, AGOSTI 5, 2026
JUMA LA 18 LA MWAKA 

KUMBUKUMBU YA HIARI YA KUTUBARUKIWA BASILIKA YA MAMA MARIA, ROMA


SOMO 1 
Yer. 31:1-7

Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.Bwana asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha. Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam, nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli, mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi.

Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni. tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu wetu.

Maana Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa. tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako mabaki ya Israeli.

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI 
Yer. 31:10-13 (K) 10

(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Lisikieni neno la Bwana,
enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali, 
mkaseme, Aliycmtawanya Israeli atamkusanya, 
na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake 
Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo, 
amemkomboa mkononi mwake
aliyekuwa hodari kuliko yeye.(K) 

Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, 
wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka, na divai; 
na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng’ombe; 
na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; 
wala hawatauzunika tena kabisa. (K)

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, 
na vijana na wazee pamoja;
maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, 
nami nitawafariji,
na kuwafurahisha waache huzuni zao. (K)


SHANGILIO
Zab 119: 105

Aleluya, aleluya,
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya.


INJILI 
Mt. 15: 21-28

Yesu aliondoka Genezareti akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema, Bwana unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukavo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment