Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATANO, AGOSTI 30, 2023


MASOMO YA MISA, JUMATANO, AGOSTI 30, 2023
JUMA LA 21 LA MWAKA 
________
SOMO I
1The. 2:9-13

Ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu. Ninyi ni mashahidi. na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa; vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia; ili mwenende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ill mwingie katikaufalme wake na utukufu wake.

Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungubila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli: litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________
WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 139: 7-12, (K) 1

(K) Ee Bwana umenichunguza na kunijua.

Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko,
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. (K)

Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)

Kama nikisema, Hakika giza litanifunika,
Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;
Giza nalo halikufichi kitu,
Bali usiku huangaza kama mehana;
Giza na mwanga kwako ni sawasawa. (K)
________
SHANGILIO
Yn. 8: 12

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, 
yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, 
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.
________
INJILI 
Mt. 23: 27-32

Yesu alisema, Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na
uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.

Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
________

Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment