MASOMO YA MISA, ALHAMISI, AGOSTI 31, 2023
JUMA LA 21 LA MWAKA
________
JUMA LA 21 LA MWAKA
________
SOMO I
1 The. 3: 7-13
Ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu yote, kwa aimani yenu. Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tuliyoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani yenu?
Basi Mungu mwenyewe, Baba yentu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze na kuwazidisha katika upendo, ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.
Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 90:3-4, 12-14, 17 (K) 14
(K) Utushibishe kwa fadhili zako, tutashangili ana kufurahi.
Wamrudisha mtu mavumbini,
Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako
Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku. (K)
Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana, urudi, hata lini?
Uwahurumie watumishi wako. (K)
Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti,
Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe. (K)
________
SHANGILIO
Yn. 14: 5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema:
Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima;
mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.
________
INJILI
Mt. 24: 42-51
Yesu aliwambia wanafunzi wake: Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
________
Copyright © 20237, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment