Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, ALHAMISI, JULAI 31, 2025




MASOMO YA MISA, 
ALHAMISI, JULAI 31, 2025
JUMA LA 17 LA MWAKA 

KUMBUKUMBU YA MT. IGNASI WA LOYOLA


SOMO 1
Kut 40: 16-21, 34-38

Musa alifanya hayo yote; kama yote Bwana aliyoagiza ndivyo alivyofanya. Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi, ile maskani ilisimamishwa. Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake. Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama Bwana alivyomwamuru Musa. Akautwaa ule ushuhuda, akautia ndani ya sanduku, akaiweka miti ya kuchukulia juu ya sanduku, akakiweka kiti cha rehema juu ya sanduku; kisha akalileta sanduku akalitia ndani ya maskani, naye akalitundika pazia la sitara, akalisitiri sanduku la ushuhuda; kama Bwana alivyomwamuru Musa.

Ndipo lile wingu likaifunikiza hema ya kukutania. na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani. Wala Musa hakuweza kuliingia hema la kukutania, kwa sababu lile wingu lilikaa juu yake, na huo utukufu wa Bwana ukaijaza maskani.

Hapo lile wingu lilipoinuliwa kutoka juu ya maskani, wana wa Israeli wakaenda mbele katika safari zao zote, bali kama lile wingu halikuinuliwa, wakati ule hawakusafiri hata siku ile lilipoinuliwa tena. Kwa maana lile wingu la Bwana lilikuwa juu ya maskani wakati wa mchana. na mlikuwa na moto ndani yake wakati wa usiku. mbele ya macho ya nyumba ya Israeli katika safari zao zote.

Neno la Mungu...Tumshukuru Mungu


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 84: 2-5, 7, 10 (K) 1

(K) Maskani zako zapendeza kama nini, ee Bwana wa majeshi.

Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
naam, na kuzikondea,
Moyo wangu na mwili wangu
Vinamlilia Mungu aliye hai. (K)

Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kito,
Alipoweka makinda yake,
Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu. (K)

Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu. (K)

Hakika siku moja katika nyua zako
Ni bora kuliko siku elfu.
Ningependa kuwa bawabu
nyumbani mwa Mungu wangu, (K)


SHANGILIO
1 Pet 1 : 25

Aleluya, aleluya, Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu. Aleluya.


INJILI
Mt. 13: 47-53

Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ufalme  wa mbinguni umefanana na juya, lilotupwa baharini, likakusanya wa kila namna; hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam. Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale. Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment