Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, ALHAMISI, AGOSTI 24, 2023


MASOMO YA MISA, ALHAMISI, AGOSTI 24, 2023
JUMA LA 20 LA MWAKA 

Sikukuu ya Mtakatifu Bartlomeo, Mtume
________

SOMO I
Ufu 21: 9-14

Malaika alinijia akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo. Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.

Neno la Bwana...Tumshukuru Mungu
________

WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 145: 10-13, 17-18 (K) 11

(K) Wacha Mungu wataunena,
utukufu wa ufalme wako, Ee Bwana.

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
na kuuhadithia uweza wako.

Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)
________

SHANGILIO
Yn 1: 49

Aleluya, aleluya,
Rabi, wewe u Mwana wa Mungu,
ndiwe Mfalme wa Israeli.
Aleluya.

________

INJILI
Yn 1: 45-51

Filipo alimwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti. Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.

Basi Yesu, akamwona Nathanaeli anakuja kwa- ke, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona. Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli. Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya. Akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu waki- kwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo
________

Copyright © 2023, "MASOMO YA MISA" published by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania. Readings reproduced by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment