"ASALI ITOKAYO MWAMBANI"
Tafakari ya kila siku
Jumanne, Julai 18, 2023
Juma la 15 la Mwaka
Jumanne, Julai 18, 2023
Juma la 15 la Mwaka
Kut 2:1-15;
Zab 69:3, 14, 30-31, 33-34;
Mt 11:20-24
AMKA NA UITIKE WITO!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya neno la Bwana naomba tuanze kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na habari za kuzaliwa kwake Musa na jinsi alivyoanza kukomboa wana wa Israeli.
Ukweli ni kwamba Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha wana wa Israeli na sasa anamtuma mkombozi kwa ajili yao kuwakomboa. Na Musa aliikubali kazi hii na leo tunasikia akianza kupingana na wowote waliokuwa wakiwapinga wana wa Israeli. Lakini cha ajabu ni kwamba wana wa Israeli ndio wanaokuwa mstari wa mbele katika kumpinga. Badala ya wao kumuona kama Mkombozi, wapo baadhi waliomuona kuwa kama kero: baadhi ya wana wa Israeli wanakataa kushirikiana naye na hata kutaka kuhatarisha uhai wa Musa.
Kukosekana kwa Ushirikiano kutamfanya Musa akimbie, akakae mafichoni na kipindi Musa akiwa mafichoni wana wa Israeli watakuwa wakiteseka-mateso ya wana wa Israeli yalizidi kuongezeka kwa sababu ya kukosekana kwa ushirikiano na Musa. Ndivyo pia ilivyotokea pale alipokuja Kristo kutukomboa. Wapo baadhi ya waliokataa kushirikiana naye na kumuona kama Kero. Hata wazee wetu wa taifa walipotaka kudai uhuru toka kwa wakoloni, wapo baadhi ya waliowakataa na kutoa ushirikiano duni. Wao walifurahia utumwa kuliko uhuru.
Sisi ndugu zangu tutambue kwamba ukosefu wetu wa ushirikiano ni sababu ya jamii yetu kushindwa na mengi. Mara nyingi tukiwaona watu wanaojitokeza kama wakombozi wetu, huwa tunaanza kuwaonea wivu kwamba wanajitafutia jina au sifa bila kutambua kwamba wivu wetu unaturudisha nyuma sisi wenyewe. Ndio maana wengi wetu ni maskini kwa sababu ya kukataa ukombozi uletwao na wenzetu.
Pia tutambue kwamba pale tunapokosa ushirikiano na viongozi wa kanisa ni hakika kujirudisha nyuma kiroho. Wengi wetu tumerudi nyuma kwa sababu ya wivu wetu. Tujifunze kushirikiana na wale wenye kutuletea ukombozi.
Katika somo la injili, Yesu anatangaza adhabu kali kwa ile miji iliyokataa kusikia sauti ya Bwana, iliyopata nafasi ya kuoneshwa mengi na Bwana lakini hiyo ikakataa kusikia sauti ya Bwana. Bwana alipotaka kuwaletea ukombozi, miji hii ilikataa. Bwana Yesu anatangaza adhabu kwa hawa. Sisi tujifunze kutumia vyema nafasi tunazopewa. Tushirikiane na viongozi wetu mbalimbali. Tutambue kwamba nafasi tuzipatazo kama za kuhudhuria ibada kila jumapili, kupokea Ekaristi wapo wanaozitafuta lakini wanazikosa. Sisi tujifunze kuzitumia vyema kwani tukionesha uzembe, hakika tutadaiwa. Tumsifu Yesu Kristo.
Sala: Bwana, nisaidie mimi niweze kuungama dhambi zangu daima. Nisaidie niweze kuwa chombo cha kuwafanya wenzagu wakurudie. Ninaomba nipokee siku zote neno lako kwa upendo na kulishirikisha kwa upendo katika hali inayo faa. Yesu, nakuamini wewe. Amina.
Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment