Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATANO, JULAI 19, 2023


MASOMO YA MISA, JUMATANO, JULAI 19, 2023
JUMA LA 15 LA MWAKA


SOMO 1
Kut. 3:1-6, 9-12

Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapa unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.

Bwana akasema: Tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 103:1-4, 6-7 (K) 8

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote. (K)

Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)

Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa. 
Akimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake. (K)


SHANGILIO
Zab. 19:8

Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.


INJILI
Mt. 11:25 – 27

Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yenyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment