Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMAPILI, JULAI 9, 2023


MASOMO YA MISA, JUMAPILI, JULAI 9, 2023
DOMINIKA YA 14 YA MWAKA


SOMO 1
Zek. 9:9-10

Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.

Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za Amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:1-2, 8-11, 14, 17 (K) 1

(K) Nitalihimidi jina lako milele na milele.

Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele. (K)

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako. (K)

Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zako zote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini. (K)


SOMO 2
Rum. 8:9, 11-13

Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili; kwa maana kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


SHANGILIO
1Sam. 3:9; Yn. 6:68
Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia; 
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.


INJILI
Mt. 11:25 – 30

Wakati ule Yesu alijibu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kuwa kwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

Neno la Bwana........Sifa kwako Ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment