Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMAMOSI, JULAI 29, 2023


MASOMO YA MISA, JUMAMOSI, JULAI 29, 2023
JUMA LA 16 LA MWAKA 

Kumbukumbu ya Familia ya Martha, Maria na Lazaro


SOMO 1
Kut. 24:3-8

Musa aliwaambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe.

Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI
Zab. 50:1-2, 5-6, 14-15 (K) 14

(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.
Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Tokea Sayuni, ukamilifu wa uzuri,
Mungu amemulika. (K)

Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu. (K)

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru;
Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. (K)


SHANGILIO
Lk. 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.


INJILI
Yn. 11:19-27

Watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.

Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; nave kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! unayasadiki hayo?

Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.

Neno la Bwana...Sifa kwako, ee Kristo

Au (2)


INJILI 
Lk. 10 : 38-42

Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamkw mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment