NOVENA YA ROHO MTAKATIFU
SIKU YA TISA, JUMAMOSI
ROHO MTAKATIFU ANATUPA MAPENDO
Maandiko Matakatifu yanatuambia ya kuwa, Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu ya
Utatu Mtakatifu, ndiye Upendo katika Baba na Mwana. Upendo hujieneza. Naye Roho
Mtakatifu aliye pendo lenyewe la Mungu, hupenda kujieneza na kujishirikisha
nasi, na kuwasha ndani yetu moto wa mapendo yake.
Roho Mtakatifu ndiye mwenye kutakatifuza roho zetu kwa neema ya utakaso.
Neema hiyo ni uzima wa Mungu, ndio huo upendo wa Mungu tunaoshirikishwa. Roho
isiyo na neema ya utakaso imetengana na Mungu, haina uzima wake, haina upendo
wake, kwa hiyo haiwezi pia kuwa na mapendo ya kweli ya jirani.
Ingawa tunaona ishara nyingi za watu kupendana kidugu hapa duniani, mapendo
hayo si mapendo ya kweli wala si kamili kama hayatokani na neema ya utakaso
rohoni mwa mtu. Kama hakuna neema ya utakaso ndani yetu, Mungu pia hayupo kati
yetu.
Roho Mtakatifu anatuunganisha na Mungu katika upendo. Pasipo na mapendo
hapana mapatano, hapana masikilizano wala mwungano. Watu wanaopendana
wanaungana na kulingana katika fikra zao na nia zao. Roho Mtakatifu anayetutia
mapendo rohoni na kutuwashia moto wa mapendo, ndiye anayetuwezesha kuwa na
mawazo ya namna moja na nia moja.
Watu wanaopendana hupenda kukaa pamoja, kuishi pamoja na kusaidiana. Roho
Mtakatifu aliye chanzo cha mapendo ya kweli hutuweka pamoja katika Kanisa lake.
Hukaa ndani yetu, hukaa katika Kanisa na kuwasha moto wa mapendo yake ndani
yetu. Roho Mtakatifu anatuwezesha kukaa kwa amani nyumbani, kazini na katika
jumuiya zetu. Basi, tumwombe sasa Roho Mtakatifu atuongezee hayo mapendo yake
ndani yetu.
1. Ewe Roho Mtakatifu, uwashe
mioyoni mwetu moto wa mapendo yako, tupate kuwapenda jirani zetu kama
tunavyotaka kupendwa nao.
W. Twakuomba utusikie
2. Udumishe ndani yetu neema
hiyo ya mapendo yako, tuwezeshe kuishi kwa amani leo na siku zote za maisha
yetu.
W. Twakuomba utusikie
3. Utujalie neema na nguvu za
kutekeleza mema yote tunayokusudia kuyatenda siku hii ya leo
W. Twakuomba utusikie
4. Uongoze nia zetu na maazimio
yetu, yalingane na juhudi zetu za kutaka kuleta mafanikio ya roho na mwili kati
yetu
W. Twakuomba utusikie
5. Utubariki, ili baada ya
maombi haya, tuwe na juhudi ya kutimiza vema zaidi wajibu wetu wa kikristu kwa
moyo mkuu
W. Twakuomba utusikie
6. Utuwezeshe kueneza mapendo
na amani kati yetu na katika jumuiya zetu za kikristu
W. Twakuomba utusikie
7. Utuwezeshe kuwa kweli chachu
ya wema na mapendano kati ya watu, ili nao wapate rehema zako kwa maombezi
yetu.
W. Twakuomba utusikie.
TUOMBE;
Ee Mungu, tunakushukuru kwa neema ulizotujalia, hata tukaweza kuifanya
ibada hii ya Novena takatifu mpaka mwisho. Utujalie mema yote tuliyoomba;
utusaidie kutekeleza yote yale tuliyokusudia kutenda. Tunaomba hayo kwa njia ya
Kristu Bwana wetu.
W. Amina.
No comments:
Post a Comment