Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

ROHO MTAKATIFU ANATUPA MWANGA


NOVENA YA ROHO MTAKATIFU 
SIKU YA NANE, IJUMAA

ROHO MTAKATIFU ANATUPA MWANGA
           
Roho Mtakatifu anaangaza akili zetu tuweze kuona ukweli wa Mungu na kuufata. Bila Roho Mtakatifu akili zetu zimo katika giza nene, wala hatuwezi kuona njia ya kutuelekeza kwa Mungu.

Mungu alipoumba ulimwengu, dunia ilikuwa giza tupu, haina kitu. Mungu alisema; “Iwe nuru”, ikawa nuru, Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema (Mwa 1;3-4) vivyo hivyo akili ya binadamu bila nuru ya mwanga wa Roho Mtakatifu, ni tupu, ina giza, haiwezi kuona mambo yanayotuelekeza kwa Mungu. Tukiwa na nuru ya Roho Mtakatifu tunaona ukweli wa Mungu jinsi ulivyo.

Roho Mtakatifu anapoijia roho ya mtu, anaiangaza akili yake iweze kuona mambo yanayofaa kwa wokovu. Naye akiisha kuiangaza akili ya mtu huimarisha utashi wake na kumwezesha kuchagua daima yaliyo mema.

Roho Mtakatifu huiangaza akili iweze kuona ukweli. Kabla ya kuwaaga mitume, Yesu aliwaambia kuwa atawapelekea mfariji mwingine atakayekaa nao siku zote. Roho wa kweli ambaye dunia haiwezi kumpokea kwa sababu hawakumfahamu, lakini wao mitume watamfahamu kwa maana atakaa nao siku zote. Yesu ametuahidi pia sisi Roho huyo akae nasi
Leo hivi duniani kuna uwongo na udanganyifu mwingi; kuna dhuluma, vita, na maovu ya kila namna. Hii ni kwa sababu dunia haijamtambua bado Roho Mtakatifu na kumpokea Yeye aliye mwanga wa dunia na asili ya kweli yote.

Mtaguso wa Pili wa Vatikano watambua ya kuwa Roho Mtakatifu anakaa katika kanisa na katika mioyo ya waumini kama katika hekalu. Roho Mtakatifu analiongoza kanisa na kulifanya liwe na umoja; analipamba na mapaji yake mabalimbali.

Tumuombe Mungu Baba ampeleke huyo Roho Mtakatifu katika kanisa lake, aliongoze na kulilinda lisipate kutengana, bali lisaidie kueneza utawala wa Mungu popote duniani.

1.       Ewe Roho Mtakatifu, utujalie kuona mwanga wa kweli yako na kuifuata
W. Twakuomba utusikie

2.       Uwape waregevu neema ya kuirudia tena njia ya kweli yako
W. Twakuomba utusikie

3.       Utuwezeshe sisi sote waamini wako tutembee siku zote katika nuru ya kweli yako na sheria zako
W. Twakuomba utusikie

4.       Utuangazie akili ya mioyo yetu tuchague daima yale yanayakupendeza
W. Twakuomba utusikie

5.       Uwape mwanga wako viongozi wetu wa dini na serikali, wapate kutuongoza kwa hekima na uchaji, wasisahau kamwe kwamba uwezo walionao unatoka kwa Mungu.
W. Twakuomba utusikie

6.       Utupe mwanga wako tuwaone watu wote kama ndugu zetu. Tuishi kindugu na kusaidiana kindugu
W. Twakuomba utusikie

7.       Ewe Roho Mtakatifu ndiwe mpatanishi wa mioyo,; tunakuomba uondoe udhalimu, uonevu, udanganyifu na maovu yote katika mioyo ya watu wote.
W. Twakuomba utusikie.

TUOMBE;
Ee Yesu Bwana wetu, uliyesema “Pasipo Mimi hamuwezi kitu” umpeleke Roho Mtakatifu atuangaze akili zetu, tupate kufahamu mapenzi yako na kuyatimiza kwa imani na uchaji. Roho Mtakatifu atuongoze katika mambo yote, yeye anayeishi na kutawala nawe pamoja na Baba daima na milele.


W. Amina

No comments:

Post a Comment