MASOMO YA MISA JUNI 9, 2023
IJUMAA, JUMA LA 9 LA MWAKA
SOMO 1
Tob. 11:5-15
Ana alikuwa amekaa kuyaelekeza macho yake njiani
hali akimtazamia mwanawe. Akamwona mbwa akija mbio; akamwambia mumewe, Lo-o-o!
Mwanao anakuja, na yule mtu aliyefuatana naye.
Rafaeli akamwambia Tobia, Najua ya kuwa baba
yako atafumbua macho yake. Basi umtie mara nyongo machoni; na imchomapo
atajifikicha; na vyamba vyeupe vitaambuka; atakuona kwa macho.
Lakini Ana alimkimbilia, akamwangukia mwanawe
shingoni, akamwambia, Mwanangu! Nimekuona; tangu sasa ni radhi nife. Wakalia
wote wawili. Tobiti naye akaondoka kwenda mlangoni, akajikwaa; lakini mwanawe
akamkimbilia, akamshika baba yake; akamtia nyongo machoni, akasema, Jipe moyo,
baba yangu. Yeye macho yake yalipoanza kuwasha aliyefikicha; navyo vyamba
vyeupe vikaambuka katika pembe za macho yake, akamwona mwanawe, akamwangukia
shingoni. Akalia, akasema, Ee Mungu umehimidiwa; na jina lako limehimidiwa
milele; na watukuzwe malaika zako watakatifu wote. Kwa maana umenirudi,
ukanihurumia; namwona mwanangu Tobia.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145:1,7-10 (K)
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Au: Aleluya.
Aleluya.
Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.
Nitamsifu Bwana muda ninaoishi,
Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai. (K)
Huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa.
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa. (K)
Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni;
Huwategemeza yatima na mjane. (K)
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, ee Sayuni,
Kizazi hata kizazi. (K)
SHANGILIO
Zab. 111 :7, 8
Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, ee Bwana,
unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya.
INJILI
Mk. 12:35-37
Yesu alipokuwa akifundisha katika hekalu,
alijibu, akasema, Husemaje waandishi ya kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi? Daudi
mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Bwana alimwambia Bwana wangu,
Uketi mkono wangu wa kuume, hata niwawekapo adui zako kuwa chini ya miguu yako.
Daudi mwenyewe asema ni Bwana; basi amekuwaje mwanawe? Na mkutano mkubwa
walikuwa wakimsikiliza kwa furaha.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment