MASOMO YA MISA JUNI 8, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 9 LA MWAKA
SOMO 1
Tob 6:11; 7:1, 9-14,8:4-8
Rafaeli alimwambia Tobiti: Ndugu yangu, leo tutatua kwa Ragueli, aliye jamaa yako: naye ana binti yake pekee, jina lake Sara. Wakafika Ekbatana, wakawasili kwenye nyumba ya Ragueli. Naye Sara akaja kuwakuta akawasalimu, nao wakamsalimu; kisha akawapeleka ndani ya nyumba. Wakawakaribisha kwa ukunjufu wakachinja kondoo dume katika kundi, wakawaandikia wingi wa nyama. Kisha Tobia akamwambia Rafaeli, Ndugu yangu Azaria, usiseme zile habari tulizoongea njiani, ili shauri liishe. Akampasha Ragueli, habari. Ragueli akamwambia Tobia, Ule unywe, na kuchangamka, maana ni wajibu wako umwoe mtoto wangu. Walakini nitakuambia kweli. Nimemwoza mtoto wangu kwa wanaume saba, na kila walipomkaribia wakafa usiku ule ule. Lakini wewe kwa sasa ujifurahishe. Tobia akamwambia, mimi sionji kitu hapa, hata mtakapofanya agano na kuagana nami. Ragueli akamjibu, vema, wewe umtwae tangu sasa kama ilivyo desturi; maana wewe u ndugu yake, naye yu wako. Naye Mungu mwenye rehema awafanikisheni katika mambo yote. Akamwita binti yake Sara akamshika mkono, akampa Tobia ili awe mke wake. Akasema, Tazama umtwae kama iamuruvyo Torati ya Musa, ukampeleke kwa baba yako. Akawabariki. Akamwita mkewe Edna, akatwaa kitabu, akaandika hati akaitia muhuri. Wakaanza kula. Na wakiisha kuwamo chumbani wote wawili, Tobia akaondoka kitandani, akasema, Ndugu yangu, ondoka, ili pamoja tumwombe Mungu atuhurumie. Ndipo Tobia alipoanza kusema, Ee Mungu wa baba zetu, umehimidiwa na jina lako takatifu tukufu limehimidiwa milele; mbingu nazo zikuhimidi, pamoja na tegemeo; na kwao umetoka uzao wote wa wanadamu. Nawe ukasema, si vema mwanaume akae peke yake; na tumfanyizie msaidizi wa kufanana naye. Na sasa Ee Bwana, simtwai huyu ndugu yangu kwa ajili ya tamaa, bali katika kweli. Uamuru nirehemiwe, hata niwahi kuona uzee pamoja naye. Sara akasema pamoja naye, Amina
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab 128:1-5
(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.
Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako.
Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako;
SHANGILIO
Yn. 8:12
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema, Bwana, yeye
anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.
INJILI
Mk. 12: 28-34
Mmoja wa waandishi alifika kwa Yesu akamwuliza,
Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza? Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii,
Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja. nawe mpende Bwana Mungu wako
kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu
zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna
amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.
Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu,
umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye; na
kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na
kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na
dhabihu zote pia. Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia,
Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea
hapo.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment