MASOMO YA MISA, JUNI 22, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 11 LA MWAKA
SOMO 1
2 Kor. 11:1 - 11
Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu
kidogo! Naam, mchukuliane nami. Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa
naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi. Lakini nachelea; kama
yule nyoka alivyomdanganya hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu,
mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo. Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine
ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili
nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye! Maana nadhani ya kuwa
mimi sikupungukiwa na kitu walicho nancho mitume walio wakuu. Lakini nijapokuwa
mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila
neno tumedhihirishwa kwenu.
Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi
mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira? Naliwanyang’anya
makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi. Nami
nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja
kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote
nalijilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena nitajilinda. Kama vile
vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa
katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya. Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi
ninyi? Mungu anajua.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 111: 1-4, 7-8 (K) 7
(K) Matendo yako Bwana ni kweli na hukumu.
Aleluya.
Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
(K)
Matendo ya Bwana ni makuu,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema. (K)
Matendo ya mikono yake ni kweli na hukumu,
Maagizo yake yote ni amini,
Yamethibitika milele na milele,
Yamefanywa katika kweli na adili. (K)
SHANGILIO
1The. 2:13
Aleluya, aleluya,
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la
wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya.
INJILI
Mt. 6:7-15
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mkiwa katika
kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa
watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana
Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba.
Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliyembinguni,
jina lako litukuzwe, ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama
huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi
tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule
mwovu.
Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba
yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala
Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment