Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 19, 2023


MASOMO YA MISA, JUNI 19, 2023
JUMATATU,  JUMA LA 11 LA MWAKA

SOMO 1
2 Kor. 6:1 – 10

Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi, msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa.
Tusiwe kwazo la namna yoyote katika jambo lolote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, ktika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aisbu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa; kama wenye huzuni, bali sikuzote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 98:1-4 (K) 2

(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)

Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

SHANGILIO
Efe. 1:17,18

Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.

INJILI
Mt. 5:38 – 42 

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment