MASOMO YA MISA, JUNI 15, 2023
ALHAMISI, JUMA LA 10 LA MWAKA
SOMO 1
2Kor. 3:15 – 4:1, 3 – 6
Hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji
huikalia mioyo yao. Lakini wakati wowote watakapomgeukia Bwana, ule utaji
huondolewa. Basi ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo
penye uhuru. Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa
Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka
utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.
Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa
jinsi tulivyopata rehema, hatulegei. Lakini ikiwa injili yetu imesitirika,
imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha
fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye
sura yake Mungu. Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni
Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu. Kwa kuwa
Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu,
atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.
Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 85:8 – 13 (K) 9
(K) Utukufu wake ukae katika nchi yetu.
Nisikie atakavyosema Mungu Bwana,
Maana atawaambia watu wake Amani,
Naam, na watauwa wake pia,
Bali wasiurudie upumbavu tena.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu. (K)
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na Amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zetu kuwa njia. (K)
SHANGILIO
Efe. 1:17, 18
Aleluya, aleluya.
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, awape roho wa
hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.
INJILI
Mt. 5:20-26
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Haki yenu
isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme
wa mbinguni.
Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na
mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake
hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu
akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na
huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele
ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kasha urudi uitoe sadaka
yako. Patina na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule
mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa
gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.
Neno la Bwana… Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment