Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA JUNI 3, 2023



MASOMO YA MISA JUNI 3, 2023
JUMAMOSI, JUMA LA 9 LA MWAKA
Kmbukumbu ya Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake, Wafiadini wa Uganda



SOMO 1
YbS 51:12-20

Wapenzi, nitamshukuru na kumsifu, na kulihimidi Jina la Bwana. Mimi nilipokuwa kijana, kabla sijasafiri bado, naliitafuta hekima kwa bidii katika sala yangu, na mbele ya hekalu nikaomba, nami hata mwisho nitazidi kuitafuta. Ikachanua kama zabibu inavyoiva, na moyo wangu ukapendezwa, na mguu wangu ukaenda katika njia iliyo sawa. Tangu ujana wangu nikafanya kuaua, nikaliinamisha sikio kidogo, nikaipokea, nikajipatia mafundisho tele. Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha. Kwa maana nalikusudi kujizoeza nayo, nikajitahidi katika yaliyo mema, wala sitatahayarishwa. Roho yangu imeshindana kwa nguvu ndani yake, na mintarafu kutenda kwangu nalikuwa mwangalifu; nikainyosha mikono yangu juu mbinguni, nikaulalamikia ujinga wangu. Nikaielekeza roho yangu moja kwa moja kwake, na katika unyofu nikaiona; tangu mwanzo nikajipatia ufahamu, na kwa hiyo sitakataliwa milele.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab 19 : 7-11

(K) Amri ya Bwana anafurahisha moyo.

Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.

Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru.

Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa.

Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali.



SHANGILIO
Zab 119:18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame, maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.


INJILI
Mk. 12:38-44

Yesu aliwaambia katika mafundisho yake: Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa.

Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment