Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUMATANO, JUNI 28, 2023


MASOMO YA MISA, JUMATANO, JUNI 28, 2023
JUMA LA 12 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MTAKATIFU IRENEO, ASKOFU NA MSHAHIDI



SOMO 1
Mwa 15: 1-12, 17-18

Neno la Bwana likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abramu akasema, Ee Bwana Mungu, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. 

Kisha akamwambia, mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, Na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akawaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua.  Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. 

Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati. 

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.




WIMBO WA KATIKATI
Zab. 105:1-4,6-9 (K) 8 

(K) Bwana analikumbuka agano lake milele. 

Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, 
Wajulisheni watu matendo yake, 
Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, 
Zitafakarini ajabu zake zote. (K)

Jisifuni kwa jina lake takatifu, 
Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. 
Mtakeni Bwana na nguvu zake, 
Utafuteni uso wake sikuzote. (K) 

Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; 
Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. 
Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; 
Duniani mwote mna hukumu zake. (K) 

Analikumbuka agano lake milele; 
Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. 
Agano alilofanya na Ibrahimu, 
uapo wake kwa Isaka. (K) 



SHANGILIO 
Zab. 147 : 12, 15 

Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, ee Yerusalemu, 
huipeleka amri yake juu ya nchi. 
Aleluya.  




INJILI
Mt 7:15-20

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.


Injili ya Bwana........Sifa kwako Ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment