Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, IJUMAA, JUNI 30, 2023


MASOMO YA MISA, IJUMAA, JUNI 30, 2023
JUMA LA 12 LA MWAKA


SOMO 1
Mwa 17:1,9-10,15-22

Abramu alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, Bwana akamtokea Abramu, akamwambia, Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume na kwenu atatahiriwa.

Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara. Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake. Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema movoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa? Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako. Mungu akasema, sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake. Na kwa habari za Ishmaeli nimekusikia, nimembariki, nitamzidisha, nami nitamwongeza sana sana. Atazaa maseyidi kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kuu. Bali agano langu nitalifanya imara kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia majira kama haya mwaka ujao. Mungu akaacha kusema naye, akapanda kutoka kwa Ibrahimu.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



WIMBO WA KATIKATI
Zab. 128 : 1-5 (K) 4

(K) Tazama, atabarikiwa hivyo yule amchaye Bwana.

Heri kila mtu amchaye Bwana,
Aendaye katika nyia yake. (K)

Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao. 
Wanao Kama miche ya mizeituni 
Wakiizunguka meza yako. (K)

Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni;
Hone uheri wa Yerusalemu siku zote za maisha yako. (K)


SHANGILIO 
MT 11:25

Aleluya, Aleluya, 
Nashukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, 
kwa kuwa mambo haya uliwaficha 
wenye hekima na akili, ukawafunulia 
watoto wachanga. 
Aleluya.



INJILI
Mt. 8:1-4

Yesu aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata. Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika. Yesu akamwambia, Angalia usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.

Injili ya Bwana........Sifa kwako Ee Kristo


Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment