Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

KUINGOA DHAMBI KUTOKA KATIKA MAISHA YETU!



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Jumamosi, Juni 17, 2023, 
Juma la 10 la Mwaka

Isa. 61:9-11
1 Sam. 2:1, 4-8 (K) 1
Lk. 2:41-51


MOYO WANGU WAMTUKUZA BWANA

Karibuni ndugu zangu katika tafakari ya neno la Mungu siku ya leo tunapoadhimisha kumbukumbu ya moyo safi wa Mama Maria. Ni kumbukumbu ambayo kwa namna ya pekee huheshimu moyo wa Mama Bikira Maria. Huu ni moyo uliohifadhi mengi katika utakatifu na usiri mkubwa. Ulipokea habari za kuwa Mama wa Mungu kwa utii mkuu kabisa, ukamtunza Yesu kwa utii mkubwa kabisa kama tunavyosikia katika injili ya leo anapojaribu kumtafua kila mahali ili ajue usalama wake, ukashiriki mateso ya Yesu hadi pale msalabani kwa uvumilivu mkubwa kabisa. Ni moyo ulioona mengi, shida na taabu lakini uliweza kuyapita yote na kupita.

Simeoni aliutabiria Moyo huu kwamba upanga utauchoma na kweli upanga mkali uliuchoma moyo wa Mama huyu alipoyaona mateso Mwanae na kukataliwa hadi kufa msalabani. Lakini moyo huu ulirudishiwa furaha kubwa hasa kwa kupata habari za ufufuko wa Yesu, zilizofuatiwa na habari za kupalizwa mbinguni na kufanywa malkia wa mbingu na huko moyo huu unafurahi siku zote milele kwani Mungu alimwezesha kuyapita mapito yote haya na sasa upo mbinguni ukifurahia kwa ushindi.

Pia ni moyo unaotuombea siku zote kwani umekuja ukitokea ulimwenguni kila nyakati za matatizo makubwa makubwa au mateso. Amekuwa akija na kutueleza cha kufanya-kweli ni msaada wa Wakristo kwani kila wakristo wakumbanapo na matatizo, umekuwa ukitokea hali akilia machozi. Kweli amekwisha tuonesha upendo mkubwa kwetu kwa kuwa malkia wa Amani, familia, afya ya wagonjwa na makimbilio ya wakosefu.

Maada ya kufurahia kwa ushindi ndiyo inayotawala masomo yetu leo. Kiitikio cha wimbo wa katikati leo kinatuambia “Moyo wangu wamtukuza Bwana” haya ni maneno aliyoyasema mama yake na Samweli baada ya kuuangalia udogo wake, utasa wake na kumpatia mtoto. Maria aliimba wimbo unaofanana na ule aliouimba mama yake samweli alipochaguliwa na Mungu kuwa mama wa mkombozi. Na huko mbinguni anaendelea kuimba wimbo wa namna hii mbele ya Mungu kutoka na ukweli wa kumfanya yeye kuwa malkia wa mbingu.

Mada hii ya furaha na ushindi tunaisikia tena katika somo la kwanza ambapo nabii anatupatia maneno ya mji wa Sioni ukifurahi kwa sababu ya baraka unazozipata kwa ujio wa watu wake, kwa sababu ya ahueni, ngekewa, kwa namna Mungu anavyomrudishia ukuu wake na baraka zake baada ya kuona magumu yote ya uhamisho. Maneno toka katika somo hili yanatumika kumwakilisha Bikira Maria, na yanatumika kana kama yanatoka mdomoni mwake kuonyesha furaha na shukrani aliyonayo Maria kwa kutukuzwa na Mungu baada ya utume wake wa kumbeba Mwana wa Mungu na kusafiri naye hapa duniani. Na sasa yuko mbinguni anafurahia.

Siku ya leo naomba tujifunze yafuatayo toka kwa huyu moyo wa mama huyu. Kwanza, ni uvumilivu. Kweli huyu mama alipitia mapito mengi kabla ya kuupata utukufu wake. Lakini ni kwa uvumilivu tu aliweza kushinda. Kama angekuwa ni mtu tu wa kwenda haraka haraka, hakika asingaliweza kufika popote. Nasi ndio hivyo hivyo. Wengi tunashindwa mitihani mingi ya kimaisha kwa sababu ya kukosa uvumilivu. Wengi tumefeli mitihani, au tumeshindwa hata kesi au tumejiingiza kwenye magumu kwa sababu ya kushindwa kutulia. Jamani, tuwe watulivu. Tukikosa subiri na utulivu hakika hatutaweza kufika mbinguni.

Pili ni kuyaweka yote mikiononi mwa Bwana. Mama Maria alikiweka kila kitu moyoni mwake na kukitafakari mbele ya Bwana. Ndivyo na sisi. Changamoto za kimaisha zipo nyingi. Tuzipeleke kwa Bwana. Tupambane kuzijibu wenyewe. Mambo mengine ni juu ya uwezo wetu.

Huu ndio moyo wa Mama yetu. Tuuige moyo huu, twende tumwombe atuombee kwa mwanae Yesu, atufundishe kuvumilia, atufundishe kumpenda Mwanae Yesu kama yeye alivyompenda. Atusaidie kwenye magonjwa mbalimbali, awe kwetu afya ya wagonjwa na kamwe asituache. Tumsifu Yesu Kristo


Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment