Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

BWANA WAKO NI NANI?



“ASALI ITOKAYO MWAMBANI”
Tafakari ya kila siku
Ijumaa, Juni 23, 2023. 
Juma la 11 la Mwaka

2Kor. 11:18, 21-30
Zab. 34: 1-6 (K) 17
Mt. 6:19-23


BWANA WAKO NI NANI?


Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunakutana na Mt.Paulo akiutetea utume wake. Wapo waliomkejeli Paulo kwamba yeye sio mtume wa kweli kama ilivyokuwa kina Petro na Yakobo na Yohane. Paulo anakuwa na ujasiri wa kueleza namna alivyojitoa sadaka kwa ajili ya Kristo zaidi hata kuliko wao.

Yeye amekuwa tayari kuipokea vyema injili ya Kristo, ameihubiri kwa wengi mchana na usiku, amekubali hata kuchapwa viboko kwa ajili ya injili, pia amepatwa na magumu mbalimbali katika utume wake, alivunjikiwa meli, alikumbana na maadui, lakini katika yote hayo alizidi kuihubiri injili bila kusita. Zaidi sana ni kwamba yeye alizidisha uvumilivu kwa ajili ya kazi ya Bwana. Alikuwa tayari kuacha yote kwa ajili ya injili.

Maisha aliyoyaishi Paulo yalionesha tabia za mtume wa kweli. Mtume wa kweli anaishi kwa ajili ya Kristo, yupo tayari kuteseka, kutoa kila alichonacho kwa ajili ya Kristo. Paulo anakuwa kielelezo kwamba hata sisi tutaweza kuwa mitume kweli kwa maisha yetu ya kujitolea. Tujitoe kwa ajili ya kazi ya Bwana. Na wale ambao tayari ni viongozi katika kanisa la Bwana watambue kwamba utume wa Kristo ni kufanana na Paulo-ni kuwa tayari kuumia kwa ajili ya Kristo. Tuepuke uvivu na kufikiria kwamba kwa kuwa viongozi katika kanisa ndio tayari tumekwishapata kila kitu; tunapaswa kufanya bidii zaidi pia, na kuwa tayari kuteseka kama ilivyotokea kwa Paulo.

Pia tusiwazuie wengine katika kanisa wenye kufanya bidii na kujitolea kwa ajili ya kazi ya Bwana. Anayefanya bidii kwa ajili ya kazi ya Bwana atiwe moyo.

Katika somo la injili, Bwana Yesu anatueleza kwamba tutumie muda wetu kujiwekea hazina mbinguni. Yesu anatoa fundisho hili akijua juu ya hatari ya tamaa ya Mwanadamu. Tamaa hii humuongoza kujilimbikizia vya dunia. Twaweza kujilimbikizia mali, marafiki, wenzi lakini vinavyotuongoza kufanya hivi sio roho wa Mungu bali ni tamaa-ni shetani ndiye mwenye kutuongoza. Lakini vya dunia vyote vinaishia hapa hapa. Na mbaya zaidi uridhi wako wa dunia waweza kuachiwa watoto au ndugu ambao huishia kuutapanya na kuutumia vibaya. Hivyo jasho lako ulilopigania kwa miaka mingi linakuja kupotezwa hivihivi.

Sisi tukumbuke kwamba mbinguni ndio makao yetu ya umilele na sio dunia. Na hivyo tuwe tayari kuyaandaa mazingira haya. Tuepuke tamaa za kidunia. Tushirikiane vyema na kanisa. Pia tutumie rasilimali zetu za dunia kuanzisha urafiki na Mwenyezi Mungu ili tuweze kufika makao haya.

Copyright ©2013-2023 ©FurKat, Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment