Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

ROHO MTAKATIFU ANATUPA NGUVU


NOVENA YA ROHO MTAKATIFU
SIKU YA SITA, JUMATANO
ROHO MTAKATIFU ANATUPA NGUVU



“Nitamuomba Baba , naye atawapelekea Mfariji mwingine atakaye kaa nanyi siku zote”. Katika maisha yenu hapa duniani tunahitaji mno kitulizo cha Mungu. Ni jambo la hekima kutafuta kitulizo hicho kwa Mungu wala si kwa viumbe; maana kitulizo kinachopatikana kwa viumbe hapa duniani hakidumu; bali kitulizo kitokacho kwa Mungu ni cha kudumu.

Roho Mtakatifu ndio kitulizo chetu cha kweli. Baba ndiye aliyetuumba, Mwana ndiye aliyetukomboa, Roho Mtakatifu ndiye aliyetutakasa mioyo yetu na kutufariji.

Kazi ya Roho Mtakatifu sio tu kuwatuliza wale walio na huzuni, bali pia kuwapa moyo wa kuvumilia taabu zozote kwa saburi.

Tunahitaji nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuweze kuishi maisha mema ya kikristu. Katika juhudi zetu za kumtumikia Mungu mara nyingi tunakutana na shida; naye Roho Mtakatifu ndie anayetufariji kwa kutupa nguvu za kupambana na matatizo yote. Maisha yetu hapa duniani yamejaa misalaba. Na misalaba hiyo hatuwezi kuichukua kwa nguvu zetu wenyewe. Roho Mtakatifu ndie anayetupa nguvu za kuvumilia. Basi, tumuombe aje kutufariji na kutupa nguvu za kuchukua msalaba wetu kwa saburi kila siku.

1.       Ee Yesu Bwana wetu, tunakusihi Wewe na Baba mumtume Roho Mtakatifu atufariji, awajalie kitulizo wale wote walio katika taabu na majonzi
W. Twakuomba utusikie

2.       Ewe Roho Mtakatifu, uwafariji wale walio katika tabu za namna zozote ili waweze kuvumilia kwa saburi mateso yao kwa faida ya Roho zao na roho za ndugu zao.
W. Twakuomba utusikie

3.       Uwafariji wale walio wagonjwa, uwajalie afya ya roho na ya mwili
W. Twakuomba utusikie

4.       Uwasaidie yatima, wajane na wote walioachwa, wasikose kupata siku kwa siku mahitaji yao ya lazima
W. Twakuomba utusikie

5.       Wajalie wale wote walio walegevu na wakosefu neema ya kuongoka na kurejea hima katika amani ya upendo wako
W. Twakuomba utusikie

6.       Uwaimarishe wale walio wema, uwajalie neema ya kudumu wasilegee katika kutenda mema leo na kesho na siku zote za maisha yao.
W. Twakuomba utusikie

7.       Utujalie  nguvu za kutafuta na kudumisha amani ya kweli katika mioyo yetu na kati ya ndugu zetu katika jumuia zetu za kikristu
W. Twakuomba utusikie

TUOMBE;
Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba neema ya Roho Mtakatifu ituangaze akili na mioyo yetu na kutujaza nguvu ya upendo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu.


W. Amina

No comments:

Post a Comment