Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

ROHO MTAKATIFU ANATUPA HEKIMA


NOVENA YA ROHO MTAKATIFU 
SIKU YA SABA, ALHAMISI

ROHO MTAKATIFU ANATUPA HEKIMA


Hekima tunayopewa na Roho Mtakatifu si sawa kama hekima inayopatikana katika ulimwengu huu.

Hekima ya Roho Mtakatifu ni ile Mtk. Paulo aliyowaambia Wakorintho ya kuwa; ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana kama wangaliielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. Lakini, ni kama yasemavyo maandiko; mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao (1Kor 2;8-9).

Mtk. Paulo alisema kama vile roho ya mtu ndiyo yenye kufahamu na kutambua yaliyo ndani yake; hivyo pia Roho Mtakatifu ndiye anayefahamu mambo ya Mungu na kutufumbulia sisi mioyoni mwetu.

Katika Sikukuu hii ya Pentekoste tunatazamia kumpokea Roho Mtakatifu. Yeye aliye hekima ya Mungu atatufumbulia siri za Mungu na ukweli wake. Ndiye atakayeamsha ndani yetu mapendo ya Yesu Msulibiwa , Mkombozi wetu. Ni yeye atakayetuongoza kutenda mema na kuacha mabaya; tunahitaji sana Roho Mtakatifu katika maisha yetu ya kila siku, tupate hekima ya kuchagua na kutenda daima yaliyo mema. Katika novena hii tuzidi kumuomba Mungu atushushie Roho Mtakatifu, atujaze na hekima yake.

1.       Ee Mungu, uwabariki viongozi wa dini na wasaidizi wao, wapate kutuongoza kwa hekima na mapendo
W. Twakuomba utusikie

2.       Ewe Roho Mtakatifu, utujalie hekima ya kutambua Mambo ya Mungu na kuyatekeleza kwa uchaji
W. Twakuomba utusikie

3.       Utujalie kuyajua mapenzi ya Mungu na kuyapokea kwa furaha
W. Twakuomba utusikie

4.       Uamshe ndani yetu mapendo ya Yesu msulibiwa , utuwezeshe kutimiza vema wajibu wetu kama wafuasi wa kweli wa Kristu Bwana wetu
W. Twakuomba utusikie

5.       Utuwezeshe kuchagua daima yaliyo mema na kuyatekeleza, tupate kulijenga na kulidumisha kanisa lako hapa duniani
W. Twakuomba utusikie

6.       Utuepushe na mafundisho yoyote yaliyo na upotovu, utujalie hekima ya kuzidi kutambua ukweli wako na mafundisho yako yaletayo wokovu
W. Twakuomba utusikie

7.       Hekima ya Roho Mtakatifu ituongoze katika satfari ya maisha yetu hapa duniani, tupate mwishowe kukurudi Wewe Muumba wetu uliye mwanzo wetu na mwisho wetu
W. Twakuomba utusiki

TUOMBE;
Ee Mungu, Baba wa utukufu, tunakuomba utupe Roho wako wa hekima, atuwezeshe kukufahamu vema, atuongoze kuishi maisha yenye kukupendeza. Utusaidie kupambana na matatizo ya maisha, tupate kuishi  maisha mema hapa duniani na mwisho tupate tunzo la heri na furaha yako huko mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.


W. Amina.

No comments:

Post a Comment