Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, MEI 17, 2023


MASOMO YA MISA, MEI 17, 2023
JUMATANO, JUMA LA 6 LA PASAKA


SOMO 1
Mdo. 17 :15, 22-18:1

Siku zile, wale waliomsindikiza Paulo wakampeleka mpaka Athene; nao wakiisha kupokea maagizo kuwapelekea Sila na Timotheo, ya kwamba wasikawie kumfuata, wakaenda zao. Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini. Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, kwa Mungu asiyejulikana.

Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote. Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao; ili wamtafute Mungu, ingawa ni kwa kupapasa-papasa, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu. Kwa maana ndani yake yeye tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu. Kama vile mmoja wetu, mtunga mashairi alivyosema, Maana sisi sote tu wazao wake.

Basi, kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu. Basi, zamani zile za ujinga Mungu alijifanya kama hazioni; bali sasa anawaagiza watu wote wa kila mahali watubu. Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu. Basi waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo. Basi hivi Paulo akaondoka akawaacha. Baadhi ya watu wakashikamana naye, wakaamini; katika hao alikuwamo Dionisio, Mwareopago, na mwanamke mmoja jina lake Damari, na watu wengine pamoja na hao. Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.




WIMBO WA KATIKATI
Zab. 148:1-2, 11-14

(K) Utukufu wako unajaza mbingu na ulimwengu.
Au: Aleluya.

Aleluya.
Msifuni Bwana kutoka mbinguni;
Msifuni katika mahali palipo juu.
Msifuni. enyi malaika zake wote;
Msifuni, majeshi yake yote. (K)

Wafalme wa dunia, na watu wote,
Wakuu, na makadhi wote wa dunia.
Vijana waume, na wanawali,
Wazee, na watoto. (K)

Na walisifu jina la Bwana,
Maana jina lake peke yake limetukuka;
Adhama yake i juu ya nchi na mbingu. (K)

Naye amewainulia watu wake pembe,
Sifa za watauwa wake wote;
Wana wa Israeli, watu walio karibu naye. (K)




SHANGILIO
Ufu. 1 : 5

Aleluya, aleluya,
Ee Kristo, yu shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.



INJILI
Yn. 16:12-15

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Bado ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasha habari.

Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.



Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment