MASOMO YA MISA, MEI 16, 2023
JUMANNE, JUMA LA 6 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 16:22-34
Siku ile, pale Filipi, wenyeji waliwakamata
Paulo na Sila, wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri
wapigwe kwa bakora. Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani,
wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii
akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo
usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za
kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu
la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka,
vifungo vya wote vikalegezwa.
Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya
kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya
kuwa wafungwa wamekimbia. Ila Paulo akapaza sauti yake kwa nguvu, akisema,
Usijidhuru, kwa maana sisi sote tupo hapa. Akataka taa ziletwe, akarukia ndani,
akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha akawaleta nje akasema,
Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana
Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako. Wakamwambia neno la Bwana, yeye na
watu wote waliomo nyumbani mwake. Akawakaribisha saa ile ile ya usiku,
akawaosha mapigo yao, kisha akabatizwa, yeye na watu wake wote wakati huo huo.
Akawaleta juu nyumbani kwake, akawaandalia chakula, akafurahi sana, yeye na
nyumba yake yote, maana amekwisha kumwamini Mungu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 138; 1-3, 7-8 (K) 7
(K) Utanyosha mkono, Ee Bwana, utaniokoa. aur
Aleluya.
Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu,
(K)
Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
Kwa maana umeikuza ahadi yako,
Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu. (K)
Utanyosha mkono juu ya hasira ya adui zangu,
Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
Usiziache kazi za mikono yako. (K)
SHANGILIO
Kol 3:1
Aleluya, aleluya,
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni
yaliyo juu, Kristo aliko, amcketi mkono wa kuume wa dunia.
Aleluya.
INJILI
Yn 16:5-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Sasa
mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye,
Unakwendapi? Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu.
Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi
nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu,
nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari
ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini
mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni
tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha
kuhukumiwa.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975,
1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, ©
Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya
Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment