MASOMO YA MISA, APRILI 30,
2024
JUMANNE, JUMA LA 5 LA PASAKA
SOMO 1
Mdo. 14 :19-28
Wayahudi walifika toka Antiokia na Ikonio,
wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji,
wakidhania ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka
pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka,
akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.
Hata walipokwisha kuhubiri Injili katika mji
ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia,
wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya
kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Na
walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na
kufunga, wakawa weka katika mikono ya Bwana waliyemwamini.
Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia. Na
baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia. Na kutoka
huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile
kazi waliyokwisha kuitimiza. Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, waka-
waeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia
Mataifa mlango wa imani. Wakaketi huko wakati usiokuwa mcha che, pamoja na
wanafunzi.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
WIMBO WA KATIKATI
Zab. 145 :10-13, 21 (K) 12
(K) Watawajulisha watu matendo yake makuu, Na
utukufu wa fahari wa zamani zote.
Au: Aleluya.
1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako,
Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. (K)
2. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
3. Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana;
Wote wenye mwili na walihimidi jina lake
takatifu milele na milele. (K)
SHANGILIO
Ufu. 1:5
Aleluya, aleluya,
Ee Kristo, yu shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa
wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.
INJILI
Yn. 14 : 27-31
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amani
nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.
Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi
naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi
kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa
nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi
sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana
kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba
alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.
Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo
Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA
MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright ©
1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of
Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha
ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.
No comments:
Post a Comment