Everyday Saint / Maisha ya Watakatifu

MASOMO YA MISA, JUNI 5, 2023


MASOMO YA MISA, JUNI 5, 2023
JUMATATU, JUMA LA 9 LA MWAKA

KUMBUKUMBU YA MT. BONIFASI (SHAHIDI)


SOMO I 
Tob. 1: 1-2; 2:1-8

Kitabu cha habari za Tobiti, bin Tobieli, bin Ananieli, bin Adueli, bin Gabaeli, wa uzao wa Asieli wa kabila ya Naftali. Zamani za Shalmanesa. mfalme wa Waashuru, huyu alichukuliwa mateka kutoka Tisbe, ulioko upande wa kuume wa Kadeshi - Naftali katika Galilaya, upande wa juu wa Asheri.

Mimi Tobiti, nilipofika nyumbani kwangu, na kurudishiwa mke wangu Ana na mwanangu Tobia, kwenye Sikukuu ya Pentekoste, iliyo siku takatifu ya juma saba, naliandaliwa chakula kizuri, nikakakaa kitako nile. Ndipo nilipoona nyama tele, nikamwambia mwanangu, Nenda ukamlete mtu maskini ye yote utakayemwona miongoni mwa ndugu zetu. amkumbukaye Bwana. Haya! nakungojea. Akarudi akasema, Baba, kuna mtu mmoja wa taifa lete amenyongwa; akatupwa sokoni. Mara, kabla sijadiriki kuonja chakula cho chote, naliondoka kwa haraka, nikaenda nikamchukua, nikampeleka katika chumba hata kuchwa kwa jua. Kisha nikarudi, nikaoga, nikala chakula changu kwa msiba, huku nikiukumbuka ule unabii wa Amosi, kusema, 

Nitageuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, Na nyimbo zenu zote kuwa vilio.

Kwa hiyo nikalia; na jua lilipokwisha kuchwa. nalikwenda nikachimba kaburi, nakamzika. Lakini jirani zangu walinidhihaki, wakasema, Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hik: ingawa alikimbia; na kumbe! anazika maiti tena.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.


WIMBO WA KATIKATI 
Zab. 112 :1-6 (K . 8)

(K) Heri mtu amchaye Bwana. au: Aleluya.

Aleluya.
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo vake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa. (K)

Nyumbani mwake mna utajiri na mali,
Na haki yake yakaa milele.
Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki. (K)

Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki.
Kwa maana hataondoshwa kamwe;
Mwenye haki atakumbukwa milele. (K)


SHANGILIO
Zab. 119:105

Aleluya, aleluya, Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu. Aleluya.



INJILI 
Mk. 12:1-12

Yesu alisema na Mafarisayo kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma, mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha -za kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua. Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu. Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.

Neno la Bwana... Sifa kwako Ee Kristo.




Copyright © 1993 T.M.P. Book Department, Tabora - Tanzania: see MASOMO YA MISA. Scripture readings from ‘Biblia Takatifu’are published and copyright © 1975, 1993 by T.M.P. Book Department, Tabora – Tanzania.© Bible Society of Kenya, © Bible Society of Tanzania.These readings are a reproduction by Furaha ya Kikatoliki: see www.fur-kat.blogspot.com.

No comments:

Post a Comment