“KWARESIMA YA UKARIMU”
Tafakari ya Kwaresima
Jumapili, Aprili 2 2023
Juma Kuu
JUMAPILI YA MATAWI
Mt 21:1-11 (Kutangaza ujio wa Bwana, Baraka ya matawi)
Isa 50: 4-7;
Zab 22: 8-9, 17-20, 23-24;
Fil 2: 6-11;
Mt 26:14 - 27:66.
MUNGU WANGU, MUNGU WANGU, MBONA UMENIACHA!
Leo ni jumapili ya matawi au jumapili ya mateso. Kipindi cha kwaresima
tulicho kianza Jumatano ya Majivu, kinapata nguvu kwa liturjia ya juma hili na
kilele chake kwa jumapili ya Pasaka. Kuanzia leo, liturjia zitakuwa zimejazwa
na ishara na alama mbali mbali: matawi, kuoshwa miguu, nk. Tusikubali ibada
hizi zipite machoni mwetu kama tu ishara ya nje pekee bali tuzichukue kama
nafasi ya kuchunguza Imani yangu, ukweli na uhusiano wangu na Mungu.
Jumapili ya matawi inaonesha shangwe juu ya Yesu akiwa anaingia Yerusalem.
Liturjia ya leo tunakumbwa na hisia mbili tofauti. Tunaanza lirtujia yetu kwa
utukufu na shangwe kuenzi jinsi Yesu alivyo ingia Yerusalemu kwa shangwe kwa
kuimba ‘hosanna, hosanna juu mbinguni’. Watu walifurahi kumuona Yesu alivyo
ingia Yerusalemu kwa shangwe, lakini hali hii inapotea taratibu baada ya kuanza
kuingia kwa undani katika masomo yetu hali inabadilika na kuwa ya kustua na
huzuni. Injili inaishia na kutundikwa kwa Yesu msalabani na Yesu analia kwa
sauti kuu nakusema “Mungu wangu mungu wangu, mbona umeniacha” na baada ya hayo
Yesu anatoa pumzi yake ya mwisho na kukata roho. Kwa muda huu watu wote hupiga
magoni kwa ukimya kutafakari kifo cha Yesu. Ni kwa jinsi ghani mambo yanaweza
kubadilika kwa muda mfupi? Ni nini kilitokea kwa watu ambao walikuwa
wakishangilia na kumsifu alivyokuwa anaingia Yerusalemu? Waliruhusuje, mtu huyu
aingie katika mateso ya msalaba na kufa?
Jibu la ndani na la kweli kabisa kwa swali hili ni kwamba Baba aliruhusu
haya yatendeke. Baba aliruhusu wamkane na kuruhusu asulubiwe. Yesu alikuwa na
uwezo wakuonesha nguvu zake za Kimungu na kukataa kukumbatia mateso ya msalaba.
Lakini hakufanya hivyo. Bali aliingia katika mateso na kukataliwa. Na wala
hakufanya kwa kujutia au akilalamika. Aliyafanya kwa mapezi yake na kuyachagua
kwa mapenzi yake.
Leo somo la kwanza linaeleza kwa undani kwamba, Yesu ni “Mtumishi wa Bwana
anayeteseka”. Alijifunza kutii kwa njia ya mateso na kwa ajili ya utii wake,
Mungu alimkweza juu kabisa. Alikuwa mtii hata kufa! Kila mkristo anatakiwa kupata
nguvu kutoka katika njia ya Kristo. “Niliwapa mgongo wangu walio nipiga” somo
la kwanza linasema. Hali ileile ambayo Yesu, mtumishi wa Mungu aliyeteseka
ikatusaidia sisi wote. Hakurudisha kisasi, hakulalamika, wala kulaumu au
kujionea huruma. Yesu aliyaangalia mateso na uchungu kama njia ya kuonesha
upendo wake kwa Baba na upendo wake kwetu.
Mateso ya Yesu, yanatuonesha hisia, tabia na mtazamo wa watu. Kwa wakati
mmoja walikuwa wamebeba matawi mikononi, wakitandaza nguo zao, wakiimba hosanna
mfalme na siku chache baadae wanakuja kupiga tena kelele, ‘asulubiwe’ kwa
Pilato. Kwanini, Mungu Baba aliruhusu haya? Kwa nini Yesu alichagua mateso na
kifo? Kwasababu ndani ya hekima kamilifu ya Baba, mateso na kifo yalikuwa kwa
lengo kubwa. Mungu aliamua kuaibisha hekima ya ulimwengu huu kwa kutumia mateso
na kifo kama njia kamili ya kupata utakatifu. Kwa tendo hili, alibadilisha uovu
mkubwa kuwa wema mkubwa. Msalaba unaninginia katikati mbele ya makanisa yetu na
nyumbani kwetu, kuonesha kwamba hakuna hata uovu uwe mkubwa kiasi ghani
unaoweza kushinda nguvu, hekima na upendo wa Mungu. Mungu ana nguvu kuliko kifo
chenyewe na Mungu ana ushindi wa mwisho hata baada ya yote kuonekana yamepotea.
Juma hili litupe matumaini ya Kimungu mara nyingi tunaweza kusukumwa kukata
tamaa na mbaya zaidi tunaweza kushawishika kukata tamaa kabisa. Hakuna ugumu,
hakuna msalaba unaweza kutushinda kama tutabaki waaminifu kwa Yesu Kristo
tukimruhusu yeye abadilishe maisha yetu kwa utukufu aliokumbatia msalabani.
Ilikuwa ni watu kama Maria, Mama yake, mtume mwaminifu kama Yohane na
wengine wachache walioweza kusimama pembeni nje ya kundi na kusimama karibu na
Yesu. Katika mwanga wa simulizi la mateso ya Yesu na matukio mengine katika
maisha ya Yesu ambayo yatasikika katika juma hili, tunapaswa kujitambua
wenyewe. Je, mimi ni Mkristo wa makundi tu au Mkristo tu tukiwa wengi? Je mi ni
Mkristo tu pale ninapo pata pato Fulani au sifa Fulani? Je, mimi ni muoga
kusimamia ukweli?
Sala: Bwana, ninapojaribiwa mpaka kukaribia kukata tamaa, naomba unipe
matumaini. Nisaidie niweze kuona uwepo wako katika kila kitu, hata katika vitu
ambavyo vinanisumbua mimi. Ninaomba juma hili kuu, libadilishe nyakati zangu za
giza na mapungufu ninapo jikabidhi kwako, Mungu wangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina
No comments:
Post a Comment